Wanamichezo SHIMIWI 2022 Waaswa Kuzingatia Kanuni za Michezo hiyo

Na Mwandishi Wetu


MASHINDANO ya Shirikisho la Michezo ya Wiraza na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2022, ambayo yanafanyika Jijini Tanga yameanza kwa wanamichezo kupewa dondoo za namna michezo hiyo itakavyoendeshwa kwa muda wa wiki mbili kuanzia Oktoba 1 hadi 15, 2022 kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Mwenyekiti wa SHIMIWI, Daniel Mwalusamba amewapa dondoo hizo wachezaji na viongozi wanaoshiriki michezo hiyo ya 36 ambayo inafanyika kwenye viwanja vya Polisi Chumbageni, Bandari, TANROADS Mizani, shule ya sekondari ya Popatlal, Usagara na Galanos kwa kushirikisha michezo ya mpira wa miguu, netiboli, kuvuta kamba, riadha, karata, bao, draft, kurusha tufe na kuendesha baiskeli.

Mwalusamba amewataka watumishi wanaoshiriki michezo hiyo kuzingatia taratibu za kazi za maofisi mwao na waendelee kuzitumia wawapo kwenye kituo hiki cha michezo na kuzingatia nidhamu ya hali ya juu.

“Tumehamishia vituo vyetu vya kazi hapa Tanga na kuwepo kwetu hapa kwenye michezo kusitufanye tukaacha maadili yetu ya kiutumishi wa umma na kuanza kufanya vitendo ambavyo ni kinyume na maadili hayo, tukumbuke Dunia ipo kwenye kiganja mtu unaweza kupigwa picha maeneo yasiyohusiana na michezo na kuandikwa maneno ambayo yataudhalilisha utumishi, mjue mtafanya watumishi wote waonekane hawana nidhamu, hivyo viongozi simamieni hili tusije kuingia huko na kuharibu taswira nzuri ya utumishi wa umma,” amesema Mwalusamba.

Hata hivyo, amewataka viongozi wa klabu zinazoshiriki kwenye michezo hii kuwasilisha kwa Kamati ya Utendaji ya SHIMIWI changamoto wanazokutana nazo kwenye hoteli walizopanga kwa kipindi choye cha michezo, ili ziweze kutatuliwa kwa wakati.

Halikadhalika, amewataka viongozi walioambatana na timu kutokuwa chanzo cha vurugu na migogoro kwenye michezo hii, wahakikishe wanasaidia vyema na kamati ya utendaji katika kutatua changamoto zozote zitakazokuwa zimetokea na kufikia muafaka mzuri, ili michezo hii iishe kwa amani na mafanikio makubwa.

Mwalusamba, pia amewapa mwongozo waamuzi watakaochezesha michezo hiyo kuzingatia sheria na kanuni ili wasiwe chanzo cha kuharibu michezo hii, na endapo atatokea kiongozi atakayetaka wapendelee timu zao kwa lengo la kumpatia bakshishi, wawaripoti kwenye uongozi wa juu wa SHIMIWI.

“Ninawaomba waamuzi wa michezo hii ikawe ya mafanikio tumeona michezo ya nyuma waamuzi walilalamikiwa hawakuchezesha kwa haki, mkiharibu mtakuwa mmeharibia hata vizazi vijavyo, ukiangalia leo sisi ni viongozi na baadaye hatutakuwepo ila michezo hii itaendelea kuwepo hivyo tusiharibu uzuri na ubora wa michezo hii,” amesema Mwalusamba.

Hata hivyo, amesisitiza ushiriki kwa wingi kwa viongozi na wachezaji wote wanaoshiriki kwenye michezo hii siku ya ufunguzi rasmi Oktoba 5, 2022 utakaofanyika kwenye uwanja wa Mkwakwani, ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.

Naye Katibu Mkuu wa SHIMIWI, Alex Temba ametoa angalizo ya matumizi ya makundi sogozi kwa kuzingatia taarifa zinazoelekezwa zikiwemo za michezo hii na si vinginevyo, ili kuepuka sintofahamu.

Wanamichezo zaidi ya 1000 wanatarajiwa kushiriki kwenye michezo hii yenye kaulimbiu ya: “Michezo hupunguza magonjwa yasiyoambukiza na kuongeza tija Mahala pa Kazi” Kazi Iendelee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *