VIONGOZI WALIOTUMIA VIBAYA FEDHA ZA LISHE WACHUKULIWE HATUA.

Angela Msimbira TAMISEMI.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa kuwachukulia hatua viongozi wote waliotumia vibaya fedha za lishe kufanyia mambo mengine badala ya kuzielekeza kwenye maswala ya lishe.

Rais Samia amesema hayo leo Septemba 30, 2022 Jijini Dodoma kwenye Hafla ya Utiaji Saini wa Mkataba ya Usimamiaji wa Shughuli za lishe na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa ambapo amesema kuwa fedha zilizoelekezwa kwenye afua za lishe zifanye kazi zake kwa ufasaha katika maeneo yao.

“Kwa wale wote waliotumia vibaya fedha za lishe wachukuliwe hatua stahiki kwa kuwa huo ni utovu wa nidhamu na hii inaonyesha kuwa hata katika miradi mingine inafanyika hivyovyo, hili halikubaliki kabisa wachukuliwe hatua kali” amesema Rais SamiaAmemuagiza Waziri wa Nchi – TAMISEMI kuwasilisha taarifa ya Halmashauri zote ambazo zimetumia fedha za lishe katika kutekeleza miradi mingine ili hatua kali ichukuliwe kwa wahusika.

Amewaagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia fedha zinazopangwa kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya lishe kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuhakikisha zinatolewa kwa wakati ili kutekeleza afua za lishe.

Amesema kuwa mpango wa lishe hautekelezwi ipasavyo, hivyo Wakuu wa Mikoa wahakikishe wanajipanga na kuongeza jitihada za kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za lishe bora na kupanga vipaombele ili kuleta tijaAidha Rais Samia amesema kuwa Serikali itaweka nguvu zaidi kwenye uboreshaji wa huduma bora za afya katika Vituo vya Afya kwa kuwekeza kwenye ununuzi wa vifaa na vifaatiba, madawa, kuajiri watumishi pamoja na kujenga nyumba za watumishi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *