MKUU WA WILAYA YA NYANG’WALE AFURAHISHWA NA HUDUMA ZA GST KATIKA MAONESHO YA TANO YA TEKINOLOJIA YA MADINI MKOANI GEITA.

Na.Samwel Mtuwa – Geita.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale Jamhuri William ambaye leo Septemba 29, 2022 ametembelea banda la GST katika Maonesho ya Tano ya Tekinolojia ya Madini mkoani Geita na kufurahia huduma mbalimbali zitolewazo na GST katika banda hilo.

Mapema alipofika katika banda la GST alipokelewa na wataalam na kupewa maelezo juu ya namna GST inavyofanya tafiti za madini nchini kwa kutumia vifaa vya kisasa.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa GST Mjiolojia Mwandamizi Melania Nyimbo , alisema kuwa mpaka sasa GST imefanya tafiti mbalimbali za madini nchini na inaendelea na tafiti hizo. Matokeo ya tafiti hizo yamepelekea kuvutia tafiti zaidi na kufanikisha kufungua migodi mbalimbali kama vile Mgodi wa Geita Gold Mine (GGM), Mgodi wa Tulawake , Mgodi wa Kabanga Nikeli , Mgodi wa Resolute na Mgodi wa Buzwagi.

Akimuelezea juu ya huduma za GST , Nyimbo alifafanua kuwa GST ina maabara ya kisasa inafanya uchunguzi wa madini katika sampuli za udongo, miamba, maji na mimea. Pia, kupitia maabara hiyo inafanya chunguzi za sampuli za mazingira na tafiti za uchenjuaji madini.

Akizungumza kuhusu taarifa zitolewazo , Nyimbo aliongeza kuwa GST ina taarifa mbalimbali za jiosayansi zilizokusanywa tokea katika vipindi mbalimbali kabla na baada ya uhuru.Taarifa hizo zinapatikana katika mfumo wa vitabu na ramani.

Akielezea Umuhimu wa taarifa hizo Nyimbo aliwaalika wachimbaji wa madini kutumia taarifa za jiosayansi zinazopatikana GST ili kuongeza ufanisi na tija katika shughuli zao.

Mapema baada ya kupokea taarifa hiyo Mkuu wa wilaya alifurahia ubora wa chungu cha kuyeyushia sampuli za dhahabu kinachozalishwa na GST kupitia Kurugenzi yake ya Huduma za Maabara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *