
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amewahakikishia Wananchi wa Jimbo hilo kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuliboresha Jiji hilo kwa kufanikisha maendeleo ya haraka katika sekta mbalimbali ikiwemo huduma za Barabara, Maji, umeme n.k
Dkt. Tulia ameyasema hayo leo Septemba 30, 2022 wakati alipokuwa akifanya ziara katika kata za Iganzo, Iwambi na Isyesye kwa lengo la kukagua miradi mbalimbali pamoja na kuzungumza na Wananchi wa maeneo hayo ili kuwaelezea mipango ya Serikali katika kuliboresha Jiji hilo.

Amesisitiza pia ya kuwa, anataka kuacha alama kubwa katika Jiji hilo kwa kipindi chake cha uongozi na tayari ndani ya kipindi cha miaka yake miwili ameshawezesha upatikanaji wa huduma nyingi muhimu ikiwemo miundombinu ya elimu, barabara, afya, umeme na maji na kuahidi kazi inaendelea.
“Wakati wa kampeni tuliwaahidi kwamba tutawaletea maendeleo, kwa upendo wa Rais wetu Mama Samia na mimi dada yenu wa Connection kazi imeanza na inaendelea hapa Mbeya Jiji. Tutajitahidi kadri tuwezavyo kutekeleza ahadi zote tulizozitoa.” Amesema Dkt. Tulia.





