MHE NDEJEMBI AWATAKA WATENDAJI SERIKALINI KUWAHAMASISHA WANANACHI KUSHIRIKI KIKAMILIFU UTEKELEZAJI WA MIRADI YA TASAF

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka watendaji wa serikali kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya TASAF nchini, ukiwemo wa ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari Budekwa wilayani Maswa ili kuunga mkono jitihada ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za kuliletea taifa maendeleo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wanafunzi na wananchi wa Kijiji cha Kiloleli wilayani Maswa, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari Budekwa unaotekelezwa na TASAF.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo, mara baada ya kukagua ujenzi wa bweni katika shule ya Sekondari Budekwa akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Kijiji cha Kiloleli wilayani Maswa.  

Mhe. Ndejembi amesema, njia pekee ya watendaji wa serikali kumuunga mkono Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi ya TASAF ni kuwahamasisha wananchi kushiriki utekelezaji wake kuanzia ngazi ya kijiji, kata, tarafa hadi wilaya ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya jitihada kubwa kupeleka mradi huo wa ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Budekwa ili kuwalinda na kuwaepusha watoto wa kike na changamoto zinazokwamisha malengo yao katika elimu.

“Mwanafunzi anapoishi katika mazingira ya shule kutokana na uwepo wa bweni, itamsaidia fikra zake zote kuzielekeza katika masomo, na hilo ndio lengo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan,” Mhe. Ndejembi amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Asengwe Kaminyoge (Wakwanza kulia) akitoa neno la utangulizi kabla ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na wanafunzi na wananchi wa Kijiji cha Kiloleli wilayani Maswa, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari Budekwa unaotekelezwa na TASAF.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bi. Prisca Kayombo    amesema Serikali imetekeleza wajibu wake kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo wa TASAF, hivyo wananchi wa Kijiji cha Kiloleli wanapaswa kuhakikisha wanashiriki kukamilisha mradi huo ili wanafunzi waweze kupata elimu bora.

Aidha, Bi. Kayombo amesema ujenzi wa bweni hilo ukikamilika utasaidia pia kupunguza changamoto ya uwepo wa mimba zisizotarajiwa kwa wanafunzi wa kike ambao baadhi yao hulazimika kukatisha masomo yao.

Mwonekano wa bweni la wasichana wa shule ya Sekondari Budekwa wilayani Maswa, linalojengwa kwa ufadhili wa TASAF kupitia miradi ya kupunguza umaskini –OPEC IV.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa bweni, Afisa Mtendaji wa Kata ya Budekwa, Bw. Masesa Madirisha amesema, mradi huo una faida kubwa katika kuboresha mazingira ya kusoma kwa watoto wa kike ambao wanapaswa kutimiza ndoto zao kama ilivyo kwa watoto wa kiume.

Kijiji cha Kiloleli ni miongoni mwa vijiji vitano vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ambavyo vinatekeleza miradi ya kupunguza umaskini ya OPEC IV Awamu ya Kwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *