
Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe amesema ameridhishwa na kasi ya utendaji ya mkandarasi anayejenga bwawa la umwagiliaji katika kijiji cha Membe wilayani Chamwino Mkoa wa Dodoma.
Mhe.Bashe amesema mkandarasi huyo ambaye ni kampuni Nakuroi Investiment Companay Ltd. anafanya kazi kwa kasi na viwango na amefuata maelekezo ya viongozi wa serikali katika ngazi zote.
Waziri Bashe amesema hayo alipofanya ziara katika kijiji cha Membe wilayani Chamwino kukagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo.

Aidha Waziri Bashe ameiagiza serikali ya kijiji cha Membe kuwatambua na kuwahakiki Wanakijiji zaidi ya 50 waliotoa mashamba yao kwa ajili ya mradi huo ili wapatiwe mashamba baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bwawa hilo pamoja na miundombinu yake.
Waziri Bashe amesisitiza uadilifu na uaminifu katika zoezi la uhakiki ili waliojitolea mashamba yao wazingatiwe kwenye kunufaika na mradi huo.
“Hii fedha inayotumika kutekeleza mradi huu ni ya Umma, hivyo sitaki vurugu, ubabaishaji, udanganyifu wala siasa kwenye utekezaji wa hili” Amesisitiza Mhe. Bashe
Waziri Bashe amesema mradi wa Bwawa la Membe unatarajiwa kumwagilia hekari 8,000 za kilimo na kuwawezesha wafugaji kunywesha mifugo yao katika eneo ambalo litaandaliwa kwa shughuli hiyo.
Mhe. Bashe amewataka Wananchi wa kijiji cha Membe na maeneo ya jirani kuacha uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na uchomaji moto kwenye milima.
Akizungumza katika eneo la mradi Mkuu wa Wilaya Chamwino Mhe. Gift Msuya amesema Mkandarasi huyo amekuwa msikivu na anafanya kazi bila usumbufu.
