GST YATOA SOMO KWA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI MKOANI GEITA JUU YA NJIA BORA ZA UTAFUTAJI MADINI

•Madini ni Sayansi.
•Uchimbaji Madini ufanyike katika maeneo yaliyothibitishwa na Utafiti wa Jiosayansi.

Na.Samwel Mtuwa – Geita.

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imewasilisha somo juu ya njia bora za kisayansi za utafutaji madini kwa wachimbaji wadogo wa Madini mkoani Geita.

Somo hilo limetolewa leo Septemba 28,2022 katika ukumbi wa EPZ wakati wa ufunguzi wa semina kwa wachimbaji wadogo iliyofungiliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Msafiri Mbibo.

Akiwasilisha mada hiyo mjiolojia mwandamizi kutoka GST , John Kalimenze aliwaeleza wachimbaji wadogo kuwa uchimbaji wa Madini hutumia gharama kubwa hivyo ni lazima ufanyike kwenye maeneo husika yaliyothibitishwa kisayansi juu ya uwepo wa Madini yatakayo chimbwa kwa faida.

Akifafanua juu ya njia bora za kisayansi za Utafutaji madini Kalimenze alizitaja njia kuu tatu ambazo zinategemeana.

Aliwasilisha kuwa moja ya njia ya utafutaji ni njia ya Jiolojia ambayo hutumika kuainisha tabia mbalimbali za miamba na madini katika eneo husika, ambapo njia hii hutumika katika maeneo yaliyojitokeza juu ya uso wa ardhi.

Akielezea juu ya njia ya Jiokemia alisema kuwa njia hii hutumika katika maeneo makubwa kwa kuchukua sampuli za miamba, Udongo , mchanga wa kwenye mito midogo, maji au mimea.

Kalimenze aliongeza kuwa sampuli hizi hupelekwa Maabara Kwa uchunguzi juu ya uwepo wa viasili vya Madini na taarifa za uchunguzi hutumika katika kuchora ramani za Jiokemia.

Ambapo njia hii ktaalam hutumika zaidi Katika maeneo ambayo miamba yake mingi imeishamong’onyoka na kuwa udongo.

Katika semina hiyo wachimbaji wadogo walielezwa juu ya njia ya Jiofizikia ambayo hutumia vifaa maalum vinavyopitishwa katika uso wa Dunia Kwa lengo la kubainisha miamba yenye asili ya usumaku.

Kwa upande wake Diwani wa Buseresere Godfrey Miti akiwa Mmoja wa washiriki wa semina hiyo ameipongeza GST Kwa kufungua ofisi mkoani Geita na kuanza kazi za upimaji wa sampuli amesema hii inatusaidia sana kupata majibu ya uhakika na kufanya uchimbaji ulio na tija bila kupoteza muda na fedha.

Mapema baada ya kumalizika kwa semina hiyo Naibu Katibu Mkuu alipata fursa ya kutembelea banda la GST.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *