Angela Msimbira, Dodoma.

Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia utoaji kiasi cha sh bilioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 8,000 vitakavyoweza kupokea wanafunzi wa ziada wa kidato cha kwanza 400,000 ambao ni zao la Elimumsingi bila ada.
Hayo yamesemwa leo Septemba 28, 2022 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza januari, 2023
Amesema fedha hizo tayari zimeshaingia kwenye akaunti za shule za sekondari 2,439 zilizoainishwa kuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya kidato cha kwanza 2023.
Amesema kwa sasa fedha hizo zimeshatumwa na kupokelewa kwenye halmashauri zote 184, kulingana na upungufu uliowasilishwa na kila Halmashauri husika.
Bashungwa amefafanua kuwa kwa mwaka 2023 takribani wanafunzi 1,148,512 wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza ambapo ni wale walioanza darasa la kwanza mwaka 2016, ambapo serikali ilianza utekelezaji sera ya Elimu msingi bila ada Disemba mwaka 2015.

Idadi ya wanafunzi waliochanguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 ilikuwa ni 907,802 ikilinganishwa na wanafunzi 422,403 waliohitimu kidato cha nne, hivyo kuhitaji kuongezeka miundombinu ya madarasa na vyoo yenye kutosheleza wanafunzi 485,399 wa ziada.
Ili kutatua changamoto hiyo, Serikali ya awamu ya sita ilitoa kiasi cha sh. Bilioni 240 zilizofanikisha ujenzi wa madarasa 12,000, shule shikizi 3,000 na mabweni 60.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza ilikuwa kubwa sana, kwa kulinganisha na miaka iliyotangulia.
Kwa mukatadha huo wanafunzi waliopo darasa la saba mwaka 2022, ndio zao la kwanza la matokeo ya Elimumsingi bila ada,”amesema Bashungwa.
Ameeleza kuwa katika hali ya kawaida matarajio ni kuwa nafasi zilizopo kwa ajili ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza, zitokane na uwepo wa shule mpya za sekondari, ujenzi wa miundombinu mipya na nafasi zilizoachwa na wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne.
“Hata hivyo, kwa mwaka 2023 wanafunzi wnaaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza wamekuwa ni wengi zaidi ukilinganisha na wanafunzi 454,902 wanaohitimu kidato cha nne 2022,”alisema Waziri Bashungwa.
Amefafanua kuwa kutokana na ongezeko la wanafunzi wanatarajia kujiunga na kidato cha kwanza kuwa kubwa mwaka 2023 ukilinganisha na nafasi 454,902 zitakazoachwa wazi na wanafunzi wa kidato cha nne.
Bashungwa amesisitiza kuwa pamoja na fedha za ujenzi wa madarasa mapya 8,000, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/22 ilitoa sh. Bilioni 108 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za kata 231.
Aidha, shule hizo ziko katika hatua mbalimbali za ukamilishaji na zikikamilika zinatarajia kupokea waafunzi Januari 2022.
