Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeipongeza Klabu ya Kriketi ya Caravan kwa kuibua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi wa mchezo huo na kuwafikisha kwenye ngazi ya kimataifa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Saidi Yakubu, leo Septemba 25, 2022 wakati kilele cha sherehe za kufunga mashindano ya Kombe la Klabu ya Kriketi ya Caravan katika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam, ambapo Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Srikanta Pradhan pia ameshiriki.

” Sisi Kama Serikali tutaendelea bila kuchoka kusaidia juhudi hizi, kama tunavyotambua tayari Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imetoa mchango mkubwa kukuzaa vipaji vya wachezaji chipukizi kwa kuwekeza fedha nyingi kwenye ujenzi wa Miundombinu” amefafanua Yakubu.
Aidha, amesisitiza kwamba kila mwaka Wizara imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya ujenzi miundombinu ya michezo ambapo sasa katika mwaka wa fedha ujao watatenga fedha kwa ajili ya mchezo huu.
Kuhusu utunzaji wa uwanja wa ili usiharibiwe kutokana na shughuli nyingine ambazo siyo za kimichezo, Yakubu amefafanua kuwa atawasiliana na mamlaka nyingine zinazosimamia uwanja huo ili uwanja huo usiharibiwe na utumike kwa ajili ya mchezo huo.



Timu ya Klabu ya Kriketi ya Caravan ni miongoni mwa klabu bora nchini yenye mchango mkubwa kwa timu ya taifa ambapo wachezaji wake watano wanachezea timu ya taifa toka mwaka 2009.
Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Calavan Adithya Kumar amesema hii ni mara ya nane kuendelea kuratibu mashindano hayo bila kukoma.
Balozi wa India nchini, Mhe Pradhan ameipongeza Klabu hiyo na kusisitiza kuwa mashindano hayo yamekuwa na mafanikio makubwa kwa kushirikiana siyo tu wahindi bali na watanzania kwa ujumla.
