Na: Debora Munisi, Dodoma.

Waziri wa Elimu, Sayansi, na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali imeandaa mkutano maalumu kwa mara nyingine wa wadau wa elimu kutoka maeneo na sekta mbalimbali nchini kote nchini.
Akizungumza na waandiahi wa habari Jijini Dodoma leo tarehe 25 Septemba 2022 Mhe Prof Adolf Mkenda amesema kuwa mkutano huo unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 26 hadi 28 Septemba 2022 Jijini Dodoma

ameeleza lengo la Mkutano huo kuwa ni kujadili Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mabadiliko ya Mitaa ya Elimu msingi.
Amesema kuwa Majadiliano hayo yatatokana na hatua iliyofikiwa na mapitio hayo kupitia kamati maalumu zilizopewa majukumu hayo.
Waziri Mkenda amesema kuwa Mkutano huo unajumuisha, Wahadhiri, Waajiri, Wadau wa Maendeleo, Taasisi za umma na Binafsi, Taasisi za Dini, Taasisi zinahusika na uendelezaji wa lugha, Wabunge, Wajumbe toka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Taasisi zisizo za Kiserikali, Jumuiya za kitaaluma, na Taasisi za Sayansi na Utafiti.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof Mkenda amesema kuwa tarehe 27 Septemba, 2022 serikali itafungua rasmi dirisha la maombi ya ufadhili wa SAMIA SCHOLARSHIPS”.
“Mtakumbuka Wizara yetu ilitoa ahadi kupitia hotuba ya bajeti ya kuanzisha programu mpya ya kutoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wahitimu bora wa kidato cha sita katika masomo ya sayansi. Siku hiyo tutatangaza rasmi Mfumo wa uombaji na vigezo” Amekaririwa Waziri Mkenda
Kadhalika, Waziri Mkenda ameukumbusha umma kuwa serikali imezindua tuzo za waandishi bunifu zijulikanazo kama Tuzo za Mwalimu Nyerere, hivyo ameendelea kukaribisha Waandishi Bunifu wa Riwaya na Mashairi kuwasilisha maandiko yao ili kuwania tuzo hizo.

Prof Mkenda amesema kuwa Mwisho wa kupokea Mawasilisho hayo ni Novemba 30, 2022 ambapo kwa taarifa zaidi kuhusu tuzo hizo na maulizo wanaweza kufuatilia katika akaunti maalumu za mitandao ya kijamii za tuzo Nyerere au mitandao na tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Taasisi ya Elimu Tanzania-TET kwa anuani ya tuzonyerere@tie.go.tz
