MHANDISI KASEKENYA AHIMIZA TEKNOLOJIA MPYA KUPENYA VIJIJINI.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akisisitiza jambo wakati akifunga maadhimisho ya 19 ya siku ya wahandisi nchini yaliyofanyika jijini Dodoma ambapo zaidi ya Wahandisi 3000 walihudhuria.

Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi, Godfrey Kasekenya amezungumzia umuhimu wa wahandisi nchini kubuni teknolojia rahisi zinazoweza kutatua changamoto za maisha ya Wananchi vijijini na hivyo kuongeza kasi ya maendeleo nchini.
Akifunga mkutano wa 19 wa Wahandisi jijini Dodoma Mhandisi, Kasekenya amesema maendeleo ya kimkakati nchini yatafikiwa endapo ubunifu na teknolojia zitawanufaisha wananchi wengi hususan waishio vijijini.
“Hakikisheni teknolojia hizi nzuri mnazoonesha mwaka hadi mwaka zinaweza kutumiwa kikamilifu na wananchi waishio vijijini na wenye kipato cha chini ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kuleta maendeleo kwa taifa zima” amesisitiza Mhandisi Kasekenya.

Baadhi ya washiriki wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya,(hayupo pichani), wakati akifunga maadhimisho ya 19 ya siku ya wahandisi nchini yaliyofanyika jijini Dodoma.

Naibu Waziri huyo ameitaka Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), kuwasilisha mapendekezo yote yaliyotolewa katika mkutano huo wa siku mbili Wizarani ili yaweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuleta tija kwa kada ya wahandisi nchini.
Amezungumzia umuhimu wa Wahandisi kuungana ili kunufaika kwa mitaji, uzoefu na hivyo kuwa na nguvu ya pamoja itakayowawezesha kukua na kukuza teknolojia ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi Eng, Balozi Aisha Amour amewataka washiriki wa mkutano huo kutumia maarifa waliyoyapata katika utekelezaji wa majukumu na kutoa elimu waliyoipata kwa wahandisi wengine ili kujenga uelewa wa pamoja katika jamii ya wahandisi nchini.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akikabidhi zawadi mbalimbali kwa washiriki mara baada ya kufunga maadhimisho ya 19 ya siku ya wahandisi nchini yaliyofanyika jijini Dodoma.


Msajili wa Bodi ya Wahandisi (ERB) Eng. Bernard Kavishe amesema zaidi ya makampuni 70 yameshiriki kuonesha bidhaa za kiteknolojia katika maonesho hayo na wahitimu 36 waliofanya vizuri katika vyuo mbalimbali vya kihandisi nchini wametunukiwa zawadi mbalimbali ikiwa ni chachu ya kuwahamasisha wanafunzi nchini kupenda fani ya uhandisi.
Mkutano huo wa siku mbili uliomalizika leo umeongozwa na kauli mbiu isemayo “Ubunifu na Uendelezaji wa Ujuzi katika kuimarisha Maendeleo Endelevu ya Uchumi wa Taifa: mtazamo wa kihandisi”

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya , akikagua moja kati ya banda la maonesho ya teknolojia mara baada ya kufunga maadhimisho ya 19 ya siku ya wahandisi nchini yaliyofanyika jijini Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *