Na Deborah Munisi. Dodoma.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji, pamoja na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso imefanya ziara na kukagua Mradi wa Maji wa Uchimbaji wa Visima Virefu unaoendelea kutekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma, (Duwasa) katika eneo la Nzuguni Jijini Dodoma
Akizungumza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Dkt.Christine Gabriel Ishengoma ameeleza kiasi cha Tsh.Bilioni 4 kutolewa zitakazotumika kusaidia katika mradi huo unaotarajiwa kumalizika.
“itasaidia wananchi hawa kuondokana na adha ya maji kwani wana imani kuwa baada ya miezi hiyo sita watakuwa wananufaika na maji haya”

Katika Ziara hiyo Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso amesema Kamati hiyo iliwapa maelekezo mahsusi ambayo yatasaidia kutatua Kero ya Maji Mkoani Dodoma na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
“Maelekezo ambayo tumetoa kwa Katibu Mkuu wa Wizara yetu ya Maji ni kuhakikisha fedha zinatoka kwa wakati Mradi huu ukamilike kwa wakati ili kuhakikisha Wana Nzuguni, Wana Kisasa, Ilazo hadi na maeneo ya Njedengwa wanapata Maji Safi na Salama.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Duwasa Mhandisi Aron Joseph wakati akiwasilisha Taarifa ya mwenendo wa Mradi huo wa Maji Safi Nzuguni kwa Kamati hiyo ya Bunge ya kilimo, mifugo na maji amesema Serikali imedhamiria kuboresha uapatikanaji wa maji kwa wakazi wa Nzuguni Jijini Dodoma ili kuondokana na adha ya maji inayowakabili wananchi hao utakaoondoa mgao wa maji maeneo ya Nzuguni, Ilazo na Kisasa.
Amesema maeneo ambayo utafiti na uchimbaji visima unaoendelea yanamilikiwa na wananchi. Mara baada ya kazi hizi kukamilika zoezi la uthamini litafanyika kwa ajili ya kulipa fidia kwa dhima ya kuyatwaa kwa matumizi ya Mamlaka.
“Maeneo ambayo utafiti na uchimbaji visima unaendelea yanamilikiwa na wananchi. Mara baada ya kazi hizi kukamilika zoezi la uthamini litafanyika kwa ajili ya kulipa fidia, ili kuyatwaa kwa matumizi ya Mamlaka”
Ametanabaisha kuwa uwepo wa mradi huo uta endelea kuongeza uzalishaji wa majisafi kutoka wastani wa lita 67.8 milioni 73.8 kwa siku na kuondoa mgao wa maji maeneo ya Nzuguni, Ilazo na Kisasa.
“Mradi huu utaongeza uzalishaji wa majisafi kutoka wastani wa lita milioni 67.8 milioni 73.8 kwa siku, sawa na ongezeko la 9% ya uzalishaji wa sasa. Ongezeko hili linapunguza 5% ya mahitaji ya sasa ya Jiji lote la Dodoma ambayo ni lita milioni 133.8 kwa siku na kutaondoa mgao wa maji Maeneo ya Nzuguni, Ilazo na Kisasa.” Amesema Mhandisi Aron Joseph.
“Mradi huu utawezesha maji yaliyokuwa yanaudumia maeneo ya Nzuguni, Ilazo na Kisasa, kupelekwa maeneo mengine ya Jiji hasa Njedengwa, Mwangaza, Mapinduzi, Iyumbu, Mlimwa, Swaswa, na Ipagala, na kuboresha hali ya upatikanaji maji na kupunguza mgao katika maeneo hayo” amesema Mhandisi Aron Joseph

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Nzuguni Diwadi wa Kata ya Nzuguni ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwajali Wananchi wa Mkoa wa Dodoma kwa kuwapatia Fedha hizo Kiasi cha Tsh Bil. 4 ambazo zitatumika kwenye utekelezaji wa mradi huo wa maji kwa lengo la kumtua Mama Ndoo Kichwani.

