SERIKALI ITAENDELEA KUTOA KIPAUMBELE WALIMU MCHEPUO WA SAYANSI

OR-TAMISEMI.

Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeliambia Bunge kuwa itaendelea kutoa kipaumbele cha kuajiri walimu wa mchepuo wa sayansi ili kuondokana na tatizo la uhaba wa walimu wa kada hiyo.

Hayo yamesemwa bungeni Septemba 21, 2022 na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. David Silinde wakati wa kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Esther Maleko(CCM).

Katika swali lake, Maleko alitaka kujua ni lini Serikali itamaliza upungufu wa walimu hususani walimu wa mchepuo wa sayansi katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Akijibu swali hilo, Mhe. Silinde amesema, Serikali kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI kila mwaka inatenga fedha kwaajili ya ujenzi wa maabara za sayansi katika shule za sekondari nchini ili kuendelea kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosoma masomo hayo.

Aidha, katika swali lake la msingi la Mhe. Maleko alitaka kujua ni lini Serikali itaanza mkakati wa kujenga hosteli katika shule za sekondari za kata.

Akijibu swali hilo, Silinde amesema Serikali inatambua umuhimu wa shule kuwa karibu na jamii.

Alisema kutokana na muktadha huo Serikali ilielekeza kujengwa kwa shule za sekondari za kata nchi nzima ili kuwezesha wanafunzi kusoma karibu na maeneo wanayoishi.

“ Kwa kutambua umuhimu wa elimu nchini wananchi wanaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kujenga hosteli katika shule za kata na kuweka utaratibu wa kuziendesha na kuzisimamia kulingana na mahitaji waliyonayo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *