SERIKALI YAELEKEZA KIWANDA KUTATUA CHANGAMOTO YA KIMAZINGIRA.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis
Hamza Khamis ameelekeza kiwanda cha nguo cha A to Z kilichpo mkoani Arusha
kikamilishe ujenzi wa mtambo wa kutibu majitaka ndani ya miezi miwili.
Ametoa maelekezo hayo jana alipofanya ziara ya kukagua na kufuatilia
utekelezaji wa maagizo ya Serikali kuhusu kuondoa changamoto ya harufu na
majitaka yanayotirirka kupita mtaro unaopita kwenye makazi ya watu.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis
Hamza Khamis akitoa maelekezo wakati wa ziara ya kikazi ya katika kiwanda cha
nguo cha A to Z ya kukagua na kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Serikali
kuhusu kuondoa changamoto ya harufu na majitaka yanayotirirka kupita mtaro
unaopita kwenye makazi ya watu.


Pia, ameelekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)
Kanda ya Kaskazini, wataalamu wa mazingira kutoka Ofisi za Mkuu wa Mkoa,
Wilaya na Halmashauri ya jiji la Arusha kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha
maeleekzo hayo yanatekelezwa.
“Hamuwezi kujua hizi harufu mbaya za haya majitaka yanayotoka hapa na
kutiririka kwenye makazi ya watu zina athari gani, sasa ninatoa miezi miwili
mkamilishe mtambo wa huu,” alisema Mhe. Khamis.
Aidha, naibu waziri huyo alisema kiwanda hicho kimekuwa kikilamikiwa na
wanachi kwa muda mrefu kwa uchafuzi wa mazingira kwa kutiririsha majitaka
katika makazi ya wananchi.
Hivyo, kutokana na hali hiyo Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kwa
kutoa maeleekzo kwa uongozi wa kiwanda kujenga mtambo wa kusafishia
majitaka kabla ya kwenda kwenye mazingira.
Akikagua ujenzi wa mtambo huo Naibu Waziri ameridhika na utekelezaji wa
mradi huo na kuwataka uongozi wa kiwanda hicho kukamilisha mara moja
mtambo huo.


Alisema Serikali inawapenda wawekezaji lakini wakati huohuo inalinda afya za
wananchi wake pamoja hifadhi ya mazingira lakini kiwanda hicho kimekuwa
kikilamikiwa na wananchi kuhusu kuchafua mazingira.
Awali Meneja wa NEMC Kanda ya Kaskazini Bw. Lewis Nzali alisema baraza hilo
limekuwa likitoa maelekezo mbalimbali ikiwemo kukipiga kiwanda hicho faini kwa
uharibifu wa mazingira.
Meneja huyo alisema kuwa kutokana na hatua hizo kiwanda cha A to Z kimeweza
kuanza kujenga mtambo wa kuchakata majitaka kabla ya kwenda kwenye
mazingira.

Sehemu ya mtambo wa zamani wa kutibu majitaka katika kiwanda cha nguo cha
A to Z mkoani Arusha ambao Serikali ilitoa maelekezo ufanyiwe maboresho.

Nzali aliongeza kwa kusema kuwa hata hivyo hatua hiyo imeleta mafanikio katika
sekta ya uwekezaji nchini kwa kuweza kuzingatia Sheria ya Mazingira ya Mwaka
2004.
Kwa upande wake Meneja wa Kiwanda cha A to Z Bw.Sylivester Kazi aliahidi
kukamilika kwa ujenzi wa mtambo huo ili kulinda afya za wananchi
wanaozunguka eneo hilo.
Mtambo huo umegharimu kiasi cha sh. Bilioni 1 ambapo kukamilika kwake
kutaondoa tatizo la majitaka kutiririka katika makazi ya wanachi na kusambaa
kwa harufu mbaya.

Mtambo mpya wa kutibu majitaka katika kiwanda cha nguo cha A to Z mkoani
Arusha unaoendelea kujengwa.


Alisema baada ya kukamilika kwa mtambo huo majitaka yote yataunganishwa na
mradi wa kuondosha majitaka wa Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Arusha
(AUWSA) hayatapita tena katika mtaro huo unaotumika sasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *