TOZO ZAPUNGUZWA, HII HAPA KAULI YA SERIKALI ILIYOTOLEWA NA WAZIRI MWIGULU BUNGENI


KAULI YA SERIKALI KUHUSU TOZO IKITOLEWA NA
MHESHIMIWA DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA MADELU (MB),
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO


Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa, katika mwaka wa fedha 2021/22,
Sheria ya Malipo ya Taifa, Sura na. 437 (National Payment System Act, Cap.
437) ilifanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2021 na
kuanzisha tozo ya miamala ya kutuma na kutoa fedha kwa njia ya simu za
mikononi yaani, Mobile Money Transaction Levy. Sambamba na tozo hii,
tulipandisha tozo kwenye mafuta kwa ajili ya kutunisha mfuko wa TARURA
na Mfuko wa Elimu ya juu. Lengo la kuanzisha tozo hizi ni kuunganisha
nguvu na umoja wa Watanzania wote katika kuiwezesha Serikali kuongeza
kasi ya kutekeleza miradi hasa ile iliyokosa fedha kutokana na ufinyu wa
bajeti ili kuwakwamua wananchi dhidi ya ukosefu wa huduma za jamii-msingi
kwa kuzingatia kuwa sura ya bejeti yetu karibu kila mahitaji ni mahitaji ya
lazima.Mahitaji ya lazima yanayolindwa kwa mfano SGR, TANROADS, Bwawa
la Umeme, REA, TARURA, Maji, Elimu, Mikopo ya Elimu ya Juu, Elimu bila
Ada, Mishahara, Deni la Taifa, Afya ni takribani 27.9 trilion na makusanyo ya
ndani ni takribani 28.01trilioni.
Mheshimiwa Spika, Serikali haina malengo ya kutoza Wananchi wake
kodi/tozo kwa ajili ya kuwapa mzigo tu, bali inalenga kuwahusisha
Watanzania wote kwa umoja wetu katika juhudi za kujikwamua kimaendeleo.
Kwa mfano, tulipofanya uamuzi huu:
a) Tulikuwa na hali mbaya sana ya barabara za vijijini zilizokosa
matengenezo kwa ufinyu wa bajeti, kadhalika, tulikuwa na vijiji
ambavyo havijawahi kuwa na barabara ya aina yeyote tangu nchi hii
ipate uhuru, akina mama wajawazito walikuwa wakibebwa kwa vitanda
kupelekwa hospitali na wengine kupoteza maisha njiani, watoto wa
shule wakibebwa na maji kwa vijito tu kukosekana kwa madaraja;
b) Tulikuwa na kilio kikubwa sana cha ukosefu wa vituo vya afya vya
kisasa vijijini, wagonjwa wote walikuwa wanalazimika kutegemea
hospitali za wilaya tu, maeneno mengine hata hospitali za wilaya
hazikuwepo, sehemu nyingine wananchi walilazimika kwenda hospitali
za mikoa jirani. Tulikuwa tunapoteza maisha ya watanzania kutokana
na umbali wa kufuata huduma za afya;
c) Tulikuwa na kilio kikubwa cha uwepo wa maboma ya madarasa na
nyumba za walimu yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi na yaliyokaa
muda mrefu bila kukamilishwa ilhali kukiwa na uhitaji mkubwa wa
madarasa kutokana na ongezeko kubwa la watoto;
2
d) Tulikuwa na kilio kikubwa cha wanafunzi waliokosa mikopo ya elimu ya
juu wapatao 26,000 wakijumuisha mwaka juzi na mwaka jana. Hawa
ni watoto wa kitanzania hasa hasa wanaotoka katika familia masikini
ambao ndoto zao za kufika chuo kikuu zilikuwa zinaishia hapo; na
e) Tulikuwa na kilio kikubwa cha maji hasa hasa vijijini, jambo hili lilikuwa
linaathiri sana shughuli za maendeleo kwa mfano kila mtoto abebe
galoni ya maji na kuibajeti kwa siku nzima, walimu kufuata maji
maeneo ya mbali, vijana wanaotaka kujenga kuingia gharama kubwa
kwa kununua maji yanayopimwa kwa ndoo pamoja na kukosekana kwa
mahitaji ya maji katika maeneo muhimu kama Hosipitalini.
Mheshimiwa Spika, makusanyo ya tozo ya miamala yameiwezesha Serikali
kutoa huduma za msingi za Wananchi wetu katika mwaka wa fedha 2021/22.
Mathalani, Serikali ilitumia jumla shilingi bilioni 7 zilitokana na tozo ya
miamala kwa ajili kujenga madarasa. Vilevile, Serikali ilitumia jumla ya
shilingi bilioni 143.7 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya ambapo kati ya
fedha hizo, shilingi bilioni 117 sawa na asilimia 81.4 ya fedha zote zilitokana
na tozo ya miamala. Kadhalika, Serikali ilitumia jumla ya shilingi bilioni 611.3
kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 221.3
zilitokana na tozo. Kwa upande wa TARURA, Serikali ilitumia jumla ya shilingi
bilioni 735.7 kwa ajili ya ujenzi wa barabara vijijini ambapo kati ya kiasi hicho
shilingi bilioni 13.5 zilitokana na tozo kwenye miamala na kiasi kingine ni tozo
kwenye mafuta.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/23, kulikuwa na mahitaji
muhimu na ya lazima ambayo yangekosa fedha kutokana na ufinyu wa
bajeti. Baadhi ya masuala muhimu ambayo yangeathiriwa kama tungefuta
kabisa chanzo hiki ni:
a) Tungeelekeza fedha za mkopo wa ECF kwenye madarasa mwaka huu,
tusingeweza kupeleka bilioni 954 kwenye kilimo zinazolenga kujenga
miundombinu ya umwagiliaji, mbegu bora pamoja na block farming.
Serikali ilitumia busara ya kiuchumi kupeleka fedha hizo kwenye sekta
za uzalishaji ili kutengeneza ajira kwa vijana, na fedha za kutoa
huduma za jamii zitafutwe kutoka kwenye tozo;
b) Tungeelekeza fedha za mkopo wa ECF kwenye ujenzi wa VETA mwaka
huu, tusingeweza kupeleka bilioni 145 kwenye mifugo, uvuvi na
wamachinga zinazolenga kujenga na kununua boti za uvuvi, kuchochea
ukuaji wa sekta ya mifugo na kujenga miundombinu na mitaji kwa
wamachinga. Katika suala hili pia, Serikali ilitumia busara ya kiuchumi
kupeleka fedha hizo kwenye sekta za uzalishaji na fedha za kutoa
huduma za jamii zitafutwe kutoka kwenye tozo;
3
c) Tungeelekeza fedha za mkopo wa AfDB kwenye ujenzi wa madarasa
na VETA mwaka huu, tusingeweza kupeleka bilioni 150 kwenye ruzuku
ya mbolea ili kuwasaidia wakulima wazalishe chakula cha kutosha kwa
ajili ya nchi yetu na kudhibiti mfumuko wa bei. Hapa pia, Serikali
ilitumia busara ya kiuchumi kupeleka fedha hizo kwenye sekta za
uzalishaji na fedha za kutoa huduma za jamii zitafutwe kutoka kwenye
tozo; na
d) Tungeamua kutotoa ruzuku ya shilingi bilioni 100 kwenye mafuta kila
mwezi tungeweza kuelekeza fedha hizo kujenga madarasa yote, VETA
na mengineyo. Hata hivyo, tungeweza kuwa na mfumuko wa bei
ambao ungeleta athari kubwa kwenye uchumi ikiwemo kupanda kwa
gharama za maisha ambazo zisingehimilika hususan kwa wananchi wa
kawaida.
Mheshimiwa Spika, Hivyo, Serikali ilitarajia kukusanya takriban shilingi
bilioni 500 kutokana na tozo ya miamala ya simu na benki na kuzielekeza
katika;
a) Ujenzi wa madarasa 8,000 nchi nzima ambapo mahitaji ya madarasa
bado yanakadiriwa kuwa 17,000;
b) Kujenga vyuo vya VETA 72 kwenye Wilaya zisizo na vyuo vya ufundi
nchini;
c) Kutekeleza mpango wa elimu bila ada kwa kidato cha tano na sita; na
d) Kuendelea na ujenzi wa zahanati na vituo vya afya na vifaa tiba katika
maeneo ambayo bado hayana huduma hizo. Nawasihi Watanzania
wote kuunga mkono juhudi hizi njema za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, mama yetu, Samia Suluhu Hassan.
Marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022
Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2021 ilifanya
marekebisho kwenye Sheria ya Malipo ya Taifa, Sura ya 437 (The National
Payment System Act, Cap 437) kwa kuanzisha tozo ya miamala ya kutuma na
kutoa fedha ambapo Kanuni ya Sheria husika (The National Payment System
(Electronic Money Transaction Levy Regulations 2021)) ilianzishwa na
kuainisha tozo kwenye miamala ya kielektroniki ya kutuma na kutoa fedha
kwa njia ya simu. Vilevile, kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022, Kanuni za
Malipo ya Taifa (The National Payment System (Electronic Money Transaction
Levy) Regulations 2021) zilifanyiwa marekebisho kwa lengo la kuongeza wigo
4
wa tozo hiyo kwa miamala yote ya kielektroniki. Marekebisho hayo
yalihusisha miamala ifuatayo ya kielektroniki ambayo inalalamikiwa;
a) Kuhamisha fedha kutoka akaunti ya Benki ya mtumiaji kwenda
mitandao ya simu;
b) Kuhamisha fedha kutoka akaunti ya Benki ya mtumiaji kwenda akaunti
nyingine ya mtumiaji ndani ya benki husika;
c) Kuhamisha fedha kutoka akaunti ya benki ya mtumiaji kwenda akaunti
ya benki nyingine;
d) Uhamishaji wa Fedha kimataifa;
e) Kutoa fedha taslimu kutoka akaunti ya simu ya mtumiaji au akaunti ya
benki kwa mkusanyaji, wakala wa mkusanyaji au mashine ya kuhesabu
fedha kielektroniki.
Mheshimiwa Spika, Kuongezwa kwa wigo wa utozaji wa tozo za miamala
kumepelekea malalamiko hasi kutoka kwa wadau. Wapo waliodhania
gharama zote hizo zimeletwa na Serikali ili hali gharama za kutuma au kutoa
fedha zimejumuisha gharama za taasisi husika na nyongeza kidogo ya
Serikali. Kwa mfano unapotoa TZS 15,000 ni TZS 2,443, Gharama ya Benki
ya Tangu zamani ni TZS 2,200 na tozo ya Serikali yaani gharama mpya ni
TZS 243, na kwenye kutuma zaidi ya milioni tatu kielektoniki (T.T) gharama
ilikuwa TZS 14,000 ambapo gharama za Mabenki tangu zamani ni TZS
10,000 na tozo ya Serikali ni TZS 4,000.
Mheshimiwa Spika, Kufuatia malalamiko hayo, Kamati Kuu ya Chama Cha
Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan
kiliielekeza Serikali kupitia upya tozo za miamala na kuzingatia maoni ya
wananchi. Wizara ya Fedha na Mipango kupitia wataalam wake wa Bajeti na
wataalam wa Sera wakiwashirikisha wadau wamefanyia kazi maelekezo ya
Chama na Maelekezo ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia upya tozo hizo.
Mheshimiwa Spika, naomba kusisitiza hapa wataalam wa Wizara ya
Fedha na Mipango wanaohusika na maswala ya Bajeti na Sera
wamefanya mapitio haya wakiwa Ofisini kama Sehemu ya
Majukumu yao ya Kila siku tofauti na taarifa zilizozungushwa kuwa
kuna tume ya watu 200 imeundwa na inatumia mabilioni ya fedha.
Napenda kuwasilisha taarifa kuwa tumefanya mapitio kama ifuatavyo:
Kupunguza mzigo wa tozo kwa jamii, Kuchochea matumizi ya miamala kwa
njia ya fedha taslimu (cash); Kurahisisha utozaji, na Kuzuia utozaji wa tozo
husika mara mbili kwa kuwa utozaji wake kwa sasa unahusisha pande zote
mbili yaani mtoaji na mpokeaji.
5
Marekebisho Yatakayofanyika
Mheshimiwa Spika, marekebisho yatakayofanyika ni kama ifuatavyo;
a) Kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya
simu (pande zote);
b) Kufuta tozo ya kuhamisha fedha ndani ya benki moja (pande zote);
c) Kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda benki
nyingine (pande zote);
d) Wafanyabiashara (merchants) hawatahusishwa kama ilivyo kwenye
kanuni za sasa;
e) Kusamehe tozo ya miamala kwenye utoaji wa fedha taslimu kupitia
wakala wa benki na ATM kwa miamala yenye thamani isiyozidi shilingi
30,000; na
f) Kupunguza gharama ya miamala kwa asilimia 10 hadi asilimia 50
kufuatana na kundi la miamala. Ikumbukwe kuwa tozo hizo ambapo
viwango vya tozo vilishushwa kwa asilimia 30 kutoka kiwango cha juu
cha shilingi 10,000 hadi kiwango cha juu cha shilingi 7,000, viwango
ambavyo vilianza kutumika tarehe 07 Septemba, 2021. Kadhalika,
Mheshimiwa Rais alisisitiza kupunguzwa zaidi tozo ambapo Wizara ya
Fedha ilipunguza tozo zaidi kwa kushusha tena kiwango cha juu kutoka
7,000 hadi 4,000.
Mheshimiwa Spika, marekebisho haya yataanza kutumika tarehe
1 Oktoba 2022.
Mheshimiwa Spika, Sambamba na hatua hiyo, Serikali inafuta utaratibu wa
kodi ya zuio inayotokana na pango kukusanywa na mpangaji na badala yake
jukumu hilo linarejeshwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa
utaratibu utakao bainishwa kwenye kanuni. Napenda kusisitiza kuwa kodi ya
zuio ya pango siyo ya mpangaji bali inapaswa kulipwa na mpangishaji
ambaye ndiye anapokea mapato kutokana na uwekezaji au biashara ya
kupangisha. Utaratibu huo umekuwa ukitumika kwa muda mrefu kwenye
nyumba za biashara na nyumba zinazopangishwa kwenye makampuni au
mashirika yanayofunga ritani za kodi.
6
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, mwisho lakini sio kwa umuhimu ni dhahiri
kwamba punguzo hili litapunguza mapato ya Serikali, naelekeza
fedha hizi zifidiwe kutokana na kubana matumizi mengineyo ndani
ya Serikali ambayo hayataathiri utekelezaji wa majukumu ya Msingi
ya mafungu husika. Namwelekeza Mlipaji Mkuu wa Serikali kukaa
na Maafisa Masuuli wote kuyaangalia upya mafungu ya matumizi
Mengineyo ili miradi ya maendeleo yote isiathirike kwa hatua hii.
Tukate kwenye chai, vitafunwa, misafara kwenye safari za ndani na
nje kwa maafisa wa Wizara zetu kama Mhe Rais alivyoelekeza,
tukate Mafunzo, Semina, Matamasha, Warsha, makundi
yanayokwenda kukagua mradi uleule kwa nyakati tofauti au
makundi yanayokwenda eneo lilelile kila mtu na gari lake (Mfano,
Wilaya ileile kila Afisa na gari peke yake, Mkoa uleule kila Kiongozi
na gari peke yake).
Mheshimiwa Spika, Naomba kuwasilisha.
Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb.)
Waziri wa Fedha na Mipango,
Septemba 20, 2022.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *