
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo yashirikiana na Wizara ya Maliasili kuitangaza Tanzania, kukuza utalii.
Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo na Wizara ya Maliasili na Utalii Septemba 16, 2022 na taasisi wadau wa Wizara hizo kutoka pande zote za Muungano wamekutana na kufanya kikao kujadili namna bora ya kutumia Utamaduni, Sanaa na Michezo kukuza utalii.
Kauli hiyo ameitoa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa baada ya kikao hicho cha pamoja ambapo amefafanua kuwa wizara yake imekuwa na matukio makubwa ambayo yanauhusiano mkubwa na Utalii.

Aidha, amesema kuna mambo ambayo wamekubaliana kwa mshikamano na kutekeleza kwa pamoja kuhakikisha kuwa sekta hizo zinakua.
Amesisitiza kuwa Kwa Ushirikiano baina ya wizara itasaidia kupeleka taifa mbele kwa kuwa sekta hizo zinategemeana.
“Sisi katika Utamaduni tunao Utamaduni wa utalii, lakini katika michezo kuna michezo na Utalii ambapo tunapokea wachezaji mbalimbali wa Kimataifa”. Ameongeza Mhe. Waziri
Amesema tayari taifa limeweza kupeleka timu nne za michezo mbalimbali kwenye kombe la dunia hivyo kwa kushirikiana na Wizara ya Utalii wanaweza kuitangaza Tanzania Kimataifa.
Katika kikao hicho wamekubaliana kuwa na kalenda inayoonesha matukio yote ya mwaka mzima ili kuweza kupanga namna bora ya kuuza utalii na kuondoka na utalii wa msimu.
Pia mawaziri hao wameelekeza watendaji kukaa na kujadili kwa kina namna bora na mikakati ya kutumia sekta hizo kukuza utali kabla kuwasilisha kwenye vikao vya juu kwa maamuzi.
Kikao hicho pia kimefanyika kufuatia maelekezo aliyoyatoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa Tamasha Utamaduni mjini Moshi ya kutaka Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kutumia sekta hizo kuitangaza Tanzania na kukuza utalii.
