MKUU WA MKOA PWANI ATOA AGIZO UDHIBITI VYANZO VYA MAJI

Na Crispin Gerald

Na Crispin Gerald

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakari Kunenge ameagiza kusitishwa kwa shughuli zote zinazohujumu vyanzo vya maji kwenye mto Ruvu pamoja na kudhibiti uvamizi wa Mto Ruvu.

Amesema kuwa shughuli zote zinazofanywa kwenye vyanzo vya Mto Ruvu kinyume na sheria zinaathiri upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Pwani na Dar.

Mhe. Kunenge pia ameeleza kuwa kulingana na utabiri wa hali ya hewa uliotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa nchini kwa kipindi hiki nchi haitaweza kupata mvua za kutosha, hivyo wananchi watumie maji kwa uangalifu na waweke akiba ya maji ya muda mrefu.

Mhe Kunenge ametoa wito huo wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kuelezea uharibifu wa vyanzo vya maji unaofanywa na wakulima na wafugaji kwenye Mto Ruvu.

“Niwatake wananchi wa Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam kuanza kutumia maji kwa uangalifu kwa kuacha kutumia maji kunyeshehea bustani na kufanya shughuli za kilimo,” amesema Mhe Kunenge.

Amefafanua kuwa hii ni tahadhari ya awali kwa wananchi wote kuhusu hali ya upatikanaji wa maji, kwa sasa bado hali ya upatikanaji wa maji iko vizuri kwenye maeneo yote.

“Lakini pia tunachukua tahadhari hizi za awali ili kuepuka athari zilizotokea mwaka jana za upungufu wa maji zilizosababishwa na shughuli za wakulima na wafugaji kwenye vyanzo vya maji,” amesema.

Mhe. Kunenge ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kushirikiana na Bonde la Wami Ruvu katika jitihada za kudhibiti shughuli zinazofanywa na wakulima na wafugaji kwenye chanzo cha Mto Ruvu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *