SATELAITI KUENDELEA KUBORESHA TAARIFA ZA HALI YA HEWA

Serikali imewahakikishia wadau wa hali ya hewa nchini kuwa itaendelea kuboresha miundombinu na watalaam wake ili kuhakikisha usahihi wa taarifa za hali ya hewa unaongezeka na kusaidia kwenye maendeleo na ukuaji wa uchumi.

Akizungumza wakati wa kufungua rasmi Kongamano la 15 la Wadau wa Satelaiti za Hali ya Hewa wa Shirika la EUMETSAT Barani Afrika, katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere, Dar es Salaam,Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Atupele Fred Mwakibete (MB) ambaye alimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Kassim Majaliwa, amesema kuwa masuala ya hali ya hewa ni mtambuka na yanagusa sekta zote hivyo kongamano hilo litakuwa muarobaini wa changamoto zinazokabili sekta hizo.

“Kwa namna ya pekee niwashukuru EUMETSAT kwa kuamua kufanyia Mkutano huu wa kimataifa nchini Tanzania, ni imani yangu kuwa siku hizi nne (4) mtachakata changamoto zote na kuja na suluhu ili sekta zote zipate ahueni katika utekelezaji wa mipango yake kwani taarifa za hali ya hewa ni muhimu sana” amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete aliendelea kwa kusema kupitia teknolojia ya satelaiti, huduma za hali ya hewa zinaendelea kuboreshwa na hivyo kuchangia katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa yanayoikumba Afrika na Dunia kwa ujumla. Aidha, ameitaka Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) kuendelea kutumia njia mbalimbali kuifikishia jamii taarifa za hali ya hewa kwa wakati.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt Agnes Kijazi amesema Kongamano hilo litajadili kwa pamoja changamoto mbalimbali na kuja na mikakati mahususi ya kuhakikisha taarifa za hali zinapatikana kwa urahisi na kwa haraka sambamba na kukidhi matakwa ya watumiaji wa taarifa hizo. Vile vile, alieleza kuwa Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano hili ni heshima kubwa kwa nchi na kuonesha mafanikio makubwa katika sekta ya hali ya hewa nchini pamoja na ushirikiano ulipo baina ya nchi za Afrika na nje ya Afrika.

“Kupitia makongamano haya nchi za Afrika zimeendelea kunufaika na uboreshaji wa utabiri wa hali ya hewa na hivyo kuchangia katika kupanga mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii”. Alisema Dkt. Kijazi

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la EUMETSAT, Dkt. Phil Evans amesema mipango ya shirika hilo ni kurusha satelaiti ya kisasa zaidi (Meteosat third Generation – MTG) mwishoni mwa mwaka huu ili kuboresha uangazi na utoaji wa taarifa za hali ya hewa hususani katika ukanda wa Afrika.

Kongamano la 15 la Wadau wa Satelaiti za Hali ya Hewa wa Shirika la EUMETSAT barani Afrika linalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 12 hadi 16 Septemba 2022, limewakutanisha Wadau wa Masuala ya Hali ya hewa kutoka nchi 59 Barani Afrika na nje ya Afrika wakiwemo Wakurugenzi wa Mamlaka za Hali ya Hewa katika Nchi za Afrika, Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Ulaya (EU).

EUMETSAT ni miongoni mwa Taasisi za kimataifa zinazoshirikiana na WMO katika shughuli za uangazi wa hali ya hewa kwa kutumia teknolojia ya satelaiti za hali ya hewa kwa nchi wanachama wa WMO.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *