CCM YAIPONGEZA DAWASA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAJI

.

Na. Noel Rukanuga-DSM

Kamati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam imeridhishwa na utendaji wa utekelezaji wa miradi ya maji inayosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ambao unagharimu zaidi ya bilioni 65.

Hatua hiyo imekuja baada ya kamati ya siasa ya Chama cha CCM Mkoa wa Dar es Salaam kufanya ziara ya kukagua mradi wa maji ulianzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) hadi Halmashauri ya Bagamoyo ili kuona kwa namna gani DAWASA wanavyotekeleza ilani ya Chama cha CCM.

Akizungumza baada ya kumaliza ziara hiyo jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Adam Ngalawa, amesema kuwa kamati imeridhishwa na utendaji wa DAWASA katika kuhakikisha wanatekeleza miradi kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma.

“Tumeongea na wananchi wamesema wanapata huduma ya maji, tunawaomba DAWASA waendelee kufanya kazi kwa ufanisi pamoja na kumaliza miradi ya maji kwa wakati” amesema Bw. Ngalawa.

Mkurugenzi wa Mradi, Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Ramadhani Mtindasi, amesema kuwa mrdai huo wa maji upo katika hatua ya mwisho ya utekelezaji ambapo hadi sasa umefikia asilimia 87.

Mhandisi Mtindasi amefafanua kuwa katika mradi huo wamelaza mbomba yenye urefu ya kilometa 1,252 pamoja na kujenga matenki ya maji matatu yenye ukubwa wa lita milioni tano kila moja ambayo yapo Vikawe, Mbweni na Tegeta A.

Amesema kuwa pia mradi umejenga vituo viwili vya kusukuma maji ambapo ukikamilika unakwenda kutoa huduma kwa wananchi zaidi ya milioni moja wanaoishi katika Mkoa wa Dar es Salaama pamoja na Pwani.

“Mradi huu unakwenda kutoa huduma Katika Manispaa ya Kinondoni, Ubungo, Kibaha pamoja na halmashauri ya Bagamoyo” amesema Mhandisi Mtindasi.

Amebainisha kuwa hukamilika kwa mradi huo ni neema kwa wakazi wa Makongo, Goba, Tegeta, Mbweni hadi Mapinga wilayani Bagamoyo.

Amesema kuwa utakapokamilika mradi, wateja 60,000 wa maeneo mbalimbali ya Changanyikeni, Vikawe, Goba, Mivumoni, Mbweni, Madale, Tegeta A, Bunju, Wazo, Ocean Bay, Salasala na Bagamoyo watanufaika.

Ameeleza kuwa kwa upande wa Bagamoyo, utahudumia wakazi wa kata za Mataya, Sanzale, Migude, Ukuni, Mtambani, Nianjema, Kimara Ng’ombe na Vikawe Bondeni.

Mhandisi Mtindasi amesaema kuwa lengo la Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni kufikia asilimia 95 ya usambazaji maji kwa upande wa mjini na asilimia 85 kwa upande wa vijijini.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe amewataka wananchi kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake kuhakikisha miundombinu ya maji inalindwa.

Mkazi wa Mabwepande, Saida Gerald Lusato ameishukuru serikali kuwafikishia huduma ya maji ambayo eneo hilo walikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *