
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inakwenda kufanya uzinduzi wa utoaji wa mikopo kupitia Mfuko wa Utamaduni ndani ya siku kumi kutoka sasa ili wasanii waweze kunufaika na mfuko huo ambao Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeuanzisha kuwanufaisha wasanii.
Hayo yamesemwa leo Septemba 7, 2022 na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa baada ya kikao na Watendaji wa Benki ya CRDB, Benki ambayo itatumika kwa ajili kutoa mikopo hiyo kwa niaba ya Serikali.
Mhe. Mchengerwa amesema uzinduzi huo utafanywa ndani ya siku kumi kuanzia sasa ambapo amefafanua kuwa mikopo hiyo haitakuwa na riba yoyote ili wasanii wengi waweze kunufaika mikopo hiyo.
Amesema katika tukio la uzinduzi wa mikopo hiyo pia Muongozo wa Uendeshaji Mfuko utazinduliwa ili vigezo na masharti ya uombaji wa mikopo vieleweke kwa waombaji.

Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ilianzisha Mfuko huo kwa lengo la utoaji wa mikopo, mafunzo na ruzuku kwa wananchi wanaojishughulisha na utengenezaji, uzalishaji na uwekezaji wa miundombinu ya Utamaduni na Sanaa pamoja na kuinua vipaji na kuzalisha kazi za ubunifu zenye kukidhi viwango vya soko la kitaifa.
Waziri Mchengerwa ametaja baadhi ya walengwa wa mfuko huo ni pamoja na watu binafsi wanaojishughulisha na kazi za Sanaa, utamaduni waliosajiliwa katika mamlaka za Serikali zinazosimamia kazi za Utamaduni na Sanaa na vikundi vya Utamaduni na Sanaa.
Wengine ni vyama vya Utamaduni na Sanaa, Mashirikisho ya Utamaduni na Sanaa, asasi za kiraia zinazojishughulisha na masuala ya Utamaduni na Sanaa pamoja na vituo vya elimu na mafunzo yanayohusiana na Utamaduni na Sanaa.

Amefafanua kuwa dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuwainua wasanii na wadau mbalimbali wanaojishughulisha Sanaa na Utamaduni ili waweze kutengeneza kazi bora zitakazoweza kuuzwa katika masoko ya kimataifa na kuinua uchumi wao na wa taifa kwa ujumla.
Na John Mapepele