BASHUNGWA AWEKA WAZI MIPANGO YA SERIKALI KUTATUA KERO ZA WALIMU NCHINI

Waziri Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa abainisha mikakati iliyowekwa na Serikali ya kutatua kumaliza kero na malalamiko ya waalimu nchini.

Bashungwa ameyasema hayo leo 08 Septemba, 2022 Jijini Dodoma wakati akielezea mikakati ya Serikali katika kuwahudumia walimu ikiwa ni moja ya kuboresha sekta ya elimu nchini.

Amesema Serikali itahakikisha Viongozi wote wanaowahudumia walimu, wakiwemo Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na watendaji wao, pamoja na Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu wanasikiliza kero za walimu kuhusu madai yao mbalimbali na yanafanyiwa kazi kulingana na Sheria, Kanuni, taratibu na Miongozo iliyopo.

“Watendaji wote wanaowahudumia walimu, wahakikishe wanakuwa karibu na walimu, wanasimamia kupokea kero na malalamiko ya walimu katika maeneo yao ya kazi na kutatua kero hizo kwa wakati” amesema Bashungwa

Aidha, Bashungwa amewaelekeza wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanandaa Mpango wa Mafunzo kulingana na mahitaji na kuhakikisha walimu walioingizwa kwenye Mpango huo wanaruhusiwa na kulipiwa stahiki za mafunzo punde wanapopata udahili.

Ameendelea kusema kuwa Serikali inaendelea kuboresha Vituo vya Walimu kwa lengo la kuwezesha ufanyikaji wa mafunzo ya walimu kazini ili kuongeza tija katika uboreshaji wa ufundishaji na ujifunzaji shuleni.

Kuhusu upungufu wa nyumba, Bashungwa amesema Serikali imeanza kutenga fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu na kipaumbele kitaanza katika maeneo ambayo ni magumu kufikika.

Amesema kwa mwaka 2022/23, Serikali imetenga Shilingi bilioni 55.57 kwa ajili ya kujenga nyuma za walimu ambapo kaya 1,916 zitanufaika huku akisisitiza kuwa utaratibu wa kutenga fedha utakuwa ukifanyika kila mwaka.

Kuhusu upandishwaji vyeo na madaraja kwa walimu, Bashungwa amewataka Tume kuhakikisha wanaziwezesha Kamati za Tume ngazi ya Wilaya, kuwapandisha walimu madaraja na kuwarekebishia vyeo kwa wakati kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.

Pia, amemwelekeza Katibu Mtendaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu, kupitia na kuchambua upandaji madaraja wa kila mwalimu, kwa lengo la kubaini stahiki halali ya daraja la mwalimu, na kuchukua hatua stahiki za kuwapandisha madaraja walimu, watakaobainika kucheleweshewa stahiki zao za madaraja.

Vile vile, Bashungwa amewaagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, kusimamia mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi za Tume na kuhakikisha linakamilika kwa wakati.

Angela Msimbira OR-TAMISEMI

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *