HALMASHAURI ZATAKIWA KUSHIRIKIANA NA TAASISI ZA DINI ZINAZOTOA HUDUMA ZA AFYA NCHINI.

OR TAMISEMI – Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amewaagiza Wakurugenzi na Waganga Wakuu wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa Mashirika ya kidini yanatoa huduma za Afya ikiwa ni pamoja na Chama Cha Madaktari Wakristo Tanzania wakati wa kutoa huduma za afya kwa wananchi.

Ametoa maelekezo hayo Jijini Dodoma, leo tarehe 05 Septemba 2022 Wakati akifunga Mkutano wa 85 wa Mwaka wa Chama Cha Madaktari Wakristo Tanzania (TCMA) uliokuwa na Mada kuu inayosema “Maboresho ya Hospitali za Kanisa katika Utoaji wa huduma za Afya na Upatikanaji wa rasilimali fedha endelefu”.

Bashungwa amesema ushirikiano na Mawasiliano hafifu ya Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu kwa taasisi za dini unarudisha nyuma maendeleo kwa jamii hivyo amewaagiza kuhakikisha wanaboresha ushirikiano taasisi hizo ili kutoa huduma bora za afya kwa jamii.

Aidha, Bashungwa amemuagiza Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ntuli Kapologwe kukaa pamoja na Chama Cha Madaktari Wakristo Tanzania kufanya mapitio ya mikataba ya Serikali kupitia Halmashauri iliyowekwa na Mashirika ya kidini Kwenye huduma za Afya.

Bashungwa amesema Serikali imeweka utaratibu wa kuwa na mikataba na mashirika ya dini kutoa huduma kwa wananchi ambapo katika mwaka wa fedha 2022/23, hospitali 87 za mashirika ya dini zina mikataba na Halmashauri kwa ajili ya kutoa huduma za Afya kwa Wananchi.

Vile vile, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inaendelea na Juhudi za kuboresha huduma za Afya ambapo katika mwaka wa fedha 2020/21 na 2021/22 Serikali imetumia zaidi ya bilioni 383 kujenga Zahanati 564, Vituo vya Afya 304 na Hospitali za wilaya 68.

Pia, ameeleza Serikali imetumia bilioni 103 kwa ajili ya ununuzi wa Vifaa tiba Kwenda Kwenye vituo vya kutoalea huduma za afya kwa mwaka 2021/22, Vivyo hivyo bilioni 69.9 zimepangwa kutumika kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *