NHC kuanza ujenzi wa mradi wa Samia Housing Scheme

Mwandishi Wetu

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limesema kwamba hivi karibuni litaanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba unaojulikana kama Samia Housing Scheme ambao unalenga katika kujenga nyumba za makazi kwa ajili ya Watanzania wenye hali ya kati na chini.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemiah Kyando Mchechu ameyasema hayo wakati akitoa mada kwenye mkutano wa siku mbili wa Wadau wa Sekta ya Miliki Tanzania ulioandaliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wadau mbalimbali wa uendelezaji miliki wakiwemo Shirika la Nyumba la Taifa na kufanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kisenga uliopo Millenium Towers, Kijitonyama Dar es Salaam.
Amesema kuwa Mradi huu wa nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya Mheshimiwa Rais na Shirika linatamani Watanzania waje wamkumbuke kwa miaka mingi ijayo. Asilimia 50 ya nyumba hizi zitajengwa Dar esSalaam, Dodoma asilimia 20 na mikoa mingine asilimia 30.
Amesema nyumba hizo zitaanza kujengwa mwezi huu wa Septemba eneo la Kawe Dar es Salaam (nyumba 500) na Medeli Jijini Dodoma (nyumba100). Mradi huu utakaotekelezwa kwa awamu utagharimu takriban Shilingi bilioni 466 sawa na dola za Kimarekani milioni 200.
Amesema lengo kuweza kuziuza kwa Sh150 milioni hadi Sh180 milioni kulingana na gharama halisi za ujenzi na nyingine Sh90 milioni pamoja na Sh50 milioni.
Amesema baada ya kukamilisha nyumba hizo sasa Shirika litajenga nyumba katika maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam yakiwemo Magomeni, Kinondoni na Ilala.
Amesema mpango huo unalenga kujenga maghorofa kwa ajili ya makazi katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya makazi ambayo yatalenga kwa watu wenye kipato cha kati na cha chini.
Amesema nyumba hizo zitawanufaisha Watanzania wengi kwasababu zitajengwa katikati ya majiji na kwamba zitajengwa katika viwanja ambavyo ni muhimu (very prime area).
Amesema katika mradi huo Shirika linatarajia kuajiri 26,000 na kulipa kodi mbalimbali za Serikali kiasi cha Shilingi bilioni 155. Kuhusu Morocco Square amesema inakaribia kukamilika na ifikapo Novemba Majengo hayo yataanza kutumika na wateja.
Kuhusu uchumi wan chi amesema mradi huo utakuza mapato ya serikali mfano mradi wa SHS 5000 unatarajiwa kutengeneza mapato ya kodi mbalimbali za serikali TZS bilioni 50 (mauzo ya nyumba) bilioni 10( ununuzi vifaa vya ujenzi), PAYE TZS 17.8 bilion, Kodi ya majengo TZS milioni 55, corporate Tax kutoka NHC na wajenzi wengine bilioni 77, VAT 60bilioni.
Aidha, itakuza sekta ya fedha kupitia mikopo ya nyumba watengenezaji, wauzaji na wakondarasi watakopa asilimia hadi 60 ambayo ni sawa na TZS 194.8 bilioni.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula akifunga Mkutano huo amesema kuwa amepigilia msumari suala la makampuni binafsi kuendesha kampeni hasi dhidi ya Serikali kuhusiana na mauzo ya viwanja vya ishirini kwa ishirini akisema kuwa mpango huo si wa haki na wenye lengo la kuwadhulumu wananchi.
Amesema mpango huo hauna maslahi kwa Watanzania masikini kwa kuwa unakiuka taratibu kuharibu miji na kuwatajirisha Makampuni machache na wamiliki wake huku ukiwaacha wakiishi maisha yasiyo na stara.
“Ninaomba sana mijadala ya upotoshaji inayoendelea mitandaoni isiendelee kwasababu inapotosha wananchi wanaelewa ndivyo sivyo…wale wanaoendelea na mjadala wa ishirini kwa ishirini, wanapotosha umma, sisi kama Wizara tumeshafuatilia, tunaweza kukubaliana kwamba kasi ya upimaji ardhi ni ndogo kwasababu hata ukiangalia ardhi imepimwa kwa asilimia 25 kwa nchi nzima na asilimia 75 yote haijapimwa, lakini viwanja vinavyosemwa… lakini tunaangilia nini kinaenda kupimwa kwa mlaji wa kawaida anachopewa na bei ya kununua,”alisema.
Anasema upande wa wa pili ambao kama serikali inawashikisha ndiyo imekuwa biashara hawazingatii taratibu kwamba katika viwanja kuna ujazo tofauti tofauti kuna vidogo vidogo vya kati na vile vikubwa.
“Hawaazingatii sheria za mipango miji. Wanajipatia kipato isivyo halali wanauza kiwanja kimoja kwa zaidi ya shilingi milioni saba wakati bei hiyo ni ya juu mara tatu ya ile ya Wizara inayouza maeneo kama hayo ambayo ni machache …tutawachukulia hatua, hatutanii,” alisema Dk Mabula.
Amefafanua kwamba kinachoifanya Serikali ichukue hatua ni ile hali ya wachache kuwaumiza wengi kwa kuwa maeneo wanayoyakata barabara hazifiki upana wa mita nne na baada ya kuwauzia wananchi wanawaelekeza kufika wizarani kwa ajili ya kupimiwa, wakati huo wameshauza na kuleta migogoro ya matumizi.
Watu hawa wanawagombanisha wananchi na Serikali kwa utaratibu huu, kisha wanawachochea kwamba Serikali inawatupa hapana si kweli, tunachokikataa ni dhuluma wanayotendewa wananchi kwa kivuli cha kuwasaidia kupata vipande hivyo vidogo vidogo vilivyo holela.
Akizungumzia Mkutano huo amesema kuwa umekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwashirikisha washiriki zaidi ya 230 kutoka ndani ya nchi huku kukiwa na michango, hoja na maoni mengi yametolewa na kupokelewa na wizara.
Kuhusu Mabenki kuangalia suala la riba, amesema kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alishalitolea maelekezo na kwamba Serikali imelichukua na inalifanyia kazi na ndiyo maana kuna baadhi ya mabenki yameanza kushusha riba.
Amesema pia Wizara imeweka utaratibu mzuri utakaowezesha kupokea maoni ya wadau mbalimbali ili kusikiliza maoni hayo na kuyafanyia kazi hasa katika kipindi hiki ambacho Wizara imeanza kufanya mabadiliko makubwa
Pia amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha wa riba katika kodi ya ardhi kwa Watanzania wote ambao wanadaiwa kodi na kwamba muda huo wa msamaha unaanzia mwezi Julai hadi Desemba.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemiah Kyando Mchechu akitoa mada kwenye mkutano wa siku mbili wa Wadau wa Sekta ya Miliki Tanzania ulioandaliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wadau mbalimbali wa uendelezaji miliki wakiwemo Shirika la Nyumba la Taifa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula akizungumza katika mkutano huo wa wadau wa sekta ya miliki kuashiria kuufunga.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi wakifuatilia jambo.

Wadau wa SEKTA ya miliki wakifuatilia mkutano huo.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi wakifuatilia jambo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *