MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA UTOAJI WA MIKOPO YA ASILIMIA 10 KUANZA KUTUMIKA

Angela Msimbira OR-TAMISEMI

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, imeanza rasmi kutumia mfumo wa kieletroniki wa kutoa mikopo ya asilimia 10 inayotokana na makusanyo ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Haya yamebainishwa leo jijini Dodoma na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe wakati akihojiwa kuhusu uanzishwaji wa mfumo huo.

Prof. Shemdoe amesema tayari Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeanza kutumia mfumo wa kutoa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ambayo hukusanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa wanawake vijana na wenye ulemavu
“Kwa sasa vikundi vinaweza kujisajili na kutuma maombi kwa njia ya mtandao.” amesema Prof. Shemdoe

Ameendelea kufafanua kuwa matumizi ya mfumo huo utatusaidia sana kuongeza uwazi wa uombaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo hiyo.

Amesema kuwa pia utasaidia kuongeza uwajibikaji, usawa na uadilifu katika kutoa huduma ya mikopo kwa vikundi husika na kusaidia kuwa na takwimu sahihi na kurahisisha utoaji wa mikopo kwa wakati

“Kupitia mfumo huu itatusaidia sana kuhakikisha kwamba waombaji wanapata mikopo kwa uwazi lakini pia kuhakikisha zile fedha zinazokopeshwa zinakuwa rahisi sana kurejeshwa.”amesisitiza Prof. Shemdoe

Prof. Shemdoe ametumia fursa hiyo kuwaelekeza maafisa maendeleo katika Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanaanza kutoa mikopo kwa kutumia mfumo huo.
“Tunataka iIdara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri zote kuanza kutumia mfumo huu wa kielektroniki ambao tumeanza kuutumia. Na pia ili kujisajili kuomba mikopo tumia anuani hii ya mikopohalmashauri.tamisemi.go.tz.”

Akifafanua zaidi kuhusu utaratibu, Prof. Shemdoe amesema kwanza inaaza kikundi kujisajili kwa kutengeneza akaunti yake na kuweka taarifa sahihi na endapo taarifa zote zitakuwa sahihi mfumo utakutumia barua pepe au ujumbe mfupi kwenye namba ya simu kwa ajili ya uhakiki na baada ya hapo utaweza ingia ndani ya mfumo ili kumalizia kujaza taarifa mbalimbali za kikundi zikiwemo taarifa za wanakikundi pamoja na viambatisho mbalimbali ikiwemo katiba na kisha kuziwasilisha taarifa za kikundi kwenye mfumo kwa ajili ya kupata hati ya usajili.

Aidha, amesema baada ya kupata hati ya usajili ambayo inapatikana pia kwa njia ya kielektroniki, kikundi kinaweza kuomba mkopo kwa kuwasilisha maombi yake kwa njia ya mfumo na kupitishwa na kamati mbalimbali za mikopo kwa kuzingatia vigezo vyote.
“Na ili uweze kufanya marejesho hakikisha unapata kumbukumbu ya malipo ya kikundi na lipa kupitia njia yoyote ya malipo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *