KAMATI YA BUNGE YA USEMI YAWAFURAHISHA WANACHI BOMA LA N’GOMBE

Wananchi wa kata ya boman’gombe wilayani kilolo, Iringa wamefurahishwa na ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Bora na Serikali za Mitaa (USEMI), iliyotembelea wilayani humo kukagua barabara ya Kidabaga – Boma la n’gombe yenye urefu wa kilomita 18.3 iliyojengwa kupitia mradi wa “Agri-Connect”.

Akiongea kwa niaba ya wananchi wa boma la n’gombe mwenyekiti wa Kijiji cha boma la n’gombe ndugu Elia Boin’gombe alisema kuwa ujio wa kamati hiyo ni faraja kubwa sana kwao kwa sababu wanaamini ujio wao ni uwepo wa Rais Samia Suluhu Hassan mwenyewe hivyo shida zao zote zitatuliwa.

“Kwakweli tunaona ni muujiza kwa kamati hii kufika hapa sababu hatujawahi kupata ugeni kutoka bungeni. Napenda kuwashukuru kwasabubu pamoja na Mheshimiwa Rais, tayari mmeshatupendelea kipande hiki cha kutoka kidabaga -boma la ngómbe kwa kiwango cha lami, sasa tunaamini ujio wenu utamaliza na hii kilomita moja iliyobaki,” alisema Boingómbe.

Kwa upande wake Mbunge wa Kilolo Mhe. Justin Nyamoga ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo alisema kuwa eneo la boma la ngómbe ni maarufu sana kwa kilimo cha mazao ya mbogamboga hivyo ujio wa barabara hiyo ni faraja kubwa kwao.

“Kutokana na changamoto ya barabara iliyokuwepo haya mazao wakati mwingine yalikuwa yanachukua hadi wiki moja kufika kidabaga, lakini tunamshukuru Mheshimwa Rais kwa sababu sasa tunapita bila shida na mazao yanafika haraka Kidabaga; na ndiyo maana tunalilia kile kipande cha kutoka kidabaga kwenda kilolo nacho kimaliziwe tuunganishe mpaka mwisho, “alisema Nyamoga.

Naye mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya USEMI Mhe. Abdallah Chaurembo (Mb), aliiagiza TARURA kukamilisha kipande cha kilomita moja kilichobaki pamoja na kuhakikisha kuwa barabara zote zitakazojengwa na TARURA zijengwe kwa kuhimili uzito wa tani 30, ili wananchi wanufaike kwa kusafirisha mazao yao kwenda sokoni kwa urahisi.

Kwa upande mwingine Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI (Afya) alisema kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI imepokea maelekezo yote ya kamati na kuahidi kuyatekeleza kwa kuanza na ujenzi wa barabara hiyo ya kilomita moja ifikapo tarehe 30 oktoba.

Aidha alisema kuwa wamechukua maelekezo ya kamati ya kujenga barabara zote za lami kwa kuanzia uzito wa tani 30 na kuendele ili wananchi wasafirishe mazao yao vizuri, na kuahidi kutekeleza maaagizo hayo.

Kamati ya kudumu ya bunge ya USEMI imemaliza ziara yake ya siku nne mkoani Iringa baada ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara za Lami za mradi wa “Agri-Connect “unaotekelezwa chini ya ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Jumuiya ya Ulaya.

Mradi huu unalenga kuwasaidia wakulima vijijini kuimarisha mnyororo wa thamani ya mazao yao hasa mazao ya Chai, Kahawa, Mbogamboga na mazao mengine yanayohitaji kusafirishwa kwa haraka toka Mashambani hadi viwandani na sokoni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *