WANANCHI WA IPALA WAISHUKURU SERIKALI KWA MIPANGO YA KUBORESHA BWAWA LA IPALA

Wananchi wa Kata ya Ipala Jijini Dodoma wameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa mipango madhubuti ya kuliboresha bwawa la Ipala ili kuwawezesha kufanya kilimo kwa mara mbili ndani ya mwaka mmoja.
Hayo yamesemwa leo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde alipotembelea eneo hilo la Ipala ambalo wananchi wamekuwa wakilitumia kwa kilimo cha mboga mboga na matunda na kuahidi kwamba serikali itahakikisha inaliboresha bwawa hilo kwa kuliongezea kina na kuweka miundo mbinu ambayo itatumiwa na wakulima na wafugaji kwa wakati mmoja.
Mhe. Mavunde ameeleza mkakati wa Wizara ya Kilimo ni kuhakikisha maji ya mvua ambayo yamekuwa yakipotea na kuharibu miundombinu yanavunwa na kuhifadhiwa vizuri kwa matumizi ya kilimo katika maeneo yenye ukame mkubwa wa mvua kama ilivyo katika maeneo ya Kanda ya Kati.


Akizungumza katika ziara hiyo,Afisa Mtendaji Mkuu wa Tume ya Umwagiliaji Nchini Ndg. Raymond Mndolwa amehakikishia wananchi wa kata ya Ipala kwamba watahakikisha Tume kwa kushirikiana na Jiji la Dodoma wanaweka miundombinu ya kuhifadhi maji ya mvua katika eneo hilo sambamba na uchimbaji wa visima ili wananchi wafanye shughuli ya kilimo mwaka mzima na hivyo kusaidia kukuza uchumi wa kaya na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Akishukuru kwa niaba ya wananchi,Diwani wa Kata ya Ipala Mhe.George Magawa ameishukuru serikali kupitia Naibu Waziri Mavunde na kuahidi ushiriki wa wananchi katika kulinda na kuutunza mradi sambamba na kujitolea kazi ndogo ndogo katika kufanikisha mradi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *