
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb), amewataka Wananchi wote kujitokeza katika zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23, 2022 ili kuisaidia Serikali kupata takwimu sahihi za Wananchi wake ili iweze kupeleka maendeleo kwa kasi stahiki.
Dkt. Tulia ameyasema hayo leo Agosti 22, 2022 wakati akizindua kituo cha Afya Nzovwe kilichopo katika Kata ya Nzovwe Jijini humo ambacho kimegharimu Shilingi Milioni 644 hadi kukamilika kwake ikiwa ni fedha za Serikali Pamoja na michango ya Wananchi.

Amesisitiza ya kuwa, ili Serikali iweze kupeleka huduma sehemu inahitaji kuwa na takwimu sahihi za watu wake ili kupata uwiano wa mahitaji hivyo endapo Wananchi watashindwa kutoa ushirikiano watakuwa wamejinyima haki yao ya kupata huduma mbalimbali ikiwemo miundombinu, afya, elimu n.k
“Wananchi wenzangu wa Mbeya, Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan anayo matamanio makubwa ya kutusaidia katika sekta mbalimbali za kimaendeleo sasa ili aweze kutekeleza hayo ni lazima ajue idadi yetu ili anapotuletea hizo neema ni lazima ajue tuko wangapi. Sasa kama tusipohesabiwa tutasaidiwaje? Niwaombe sana tujitokeze kesho Agosti 23, 2022 kwa wingi na tuendelee kuwaelimisha na wengine kuhusu umuhimu wa sensa” amesema Dkt. Tulia


