Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha wanaziba mianya ya rushwa kwenye vyanzo vya mapato vya Serikali vilivyobuniwa kimkakati ili kuongeza pato la taifa litakalotumika kuleta maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta za kilimo, afya, madini, nishati, utalii na miundombinu.

Mhe. Jenista ameyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya ‘Intermediate Investigation Course’ kwa Wakuu wa Vitengo wa TAKUKURU Makao Makuu, Mikoa na Wilaya yaliyofanyika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Pwani.
Mhe. Jenista amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kubuni vyanzo vipya vya ukusanyaji mapato ili vitumike kuleta maendeleo nchini, lakini kwenye jambo lolote zuri linapofanywa na Serikali rushwa huwa inajipenyeza hivyo, ni wajibu wa kila mtumishi wa TAKUKURU kujipanga na kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kuzuia rushwa isikwamishe mipango ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.

“Watumishi wa TAKUKURU tumieni vizuri mafunzo haya mliyoyapata kutekeleza kikamilifu jukumu lenu la kuzuia na kupambana na rushwa kwenye vyanzo vyote vya mapato na miradi ya kimkakati ambayo Serikali imebuni kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Akizungumzia eneo lingine ambalo watumishi wa TAKUKURU wanatakiwa kulipa uzito katika ufuatiliaji, Waziri Jenista amesema ni eneo la fursa za biashara na uwekezaji ambazo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akizitafuta kwa juhudi kubwa ili ziwe na tija na manufaa katika maendeleo ya taifa.

“Mhe. Rais ana mapenzi mema na taifa letu na ndio maana amekuwa mstari wa mbele kutafuta fursa za biashara na uwekezaji ili watanzania wanufaike na fursa hizo kwa kupata huduma bora na kuongeza kipato chao, hivyo hatuna budi kumuunga mkono kwa kutekeleza majukumu yetu kikamilifu katika mapambano dhidi rushwa ili kuwavutia wawekezaji kuwekeza nchini.” Mhe. Jenista ameongeza.
Waziri Jenista ameongeza kuwa, rushwa isipozuiwa katika sekta ya uwekezaji ni wazi kuwa wawekezaji watakosa imani na kushindwa kuwekeza nchini, hivyo taifa litakosa mapato.
Aidha, Mhe. Jenista ameitaka TAKUKURU kufanya ufuatiliaji na kuchukua hatua stahiki kwa watendaji wasiotenda haki kwa watumishi wanaowangoza, ikiwa ni pamoja na wale wanaoshindwa kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kushughulikia stahiki za watumishi wa umma.

“Tabia za unyanyasaji, upendeleo na mambo mengine yanayokwamisha watumishi wa umma kupewa stahiki zao hazitovumilika, TAKUKURU nawaagiza kufuatilia jambo hili kwa karibu ili watumishi wa umma wasinyimwe haki zao za msingi kama ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiagiza mara kwa mara ili kuongeza morari ya watumishi kufanya kazi kwa bidIi na uadilifu.” Mhe. Jenista amesisitiza.
Awali, akimkaribisha Waziri Jenista kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi wa TAKUKURU, CP Salum Hamduni amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha bajeti iliyowezesha watumishi hao kushiriki mafunzo hayo.

“Mafunzo kama haya mara ya mwisho yalifanyika mwaka 2011 kutokana na ufinyu wa bajeti, lakini Mhe. Rais kwa kuwa aliona kuna umuhimu mkubwa wa watumishi hawa kushiriki mafunzo aliidhinisha bajeti.” CP Hamduni amefafanua.
Mafunzo hayo yamefanyika ili kukidhi matakwa ya muundo wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na yamehudhuriwa na Wakuu wa Vitengo wa TAKUKURU wapatao 100 kutoka Makao Makuu, mikoani na wilayani.


