Tanzania inatarajiwa kuwa Mwenyeji wa Mikutano ya Mabaraza ya Mawaziri wa Maji wa Bonde la Mto Nile Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupewa heshima ya kuandaa mikutano ya Mabaraza ya Mawaziri wa Maji wa Bonde la Mto Nile.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Amthony Sanga amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Taasisi ya Mpito ya Nile (Nile Basin Initiative – NBI) zinaandaa mikutano ya Mabaraza ya Mawaziri wa Bonde la Mto Nile itakayofanyika Hyatt Regency (The Kilimanjaro), Jijini Dar es Salaam Tanzania kuanzia tarehe 18 -19 Agosti, 2022.

Mhandisi Sanga ameitaja mikutano hiyo ni Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa ENSAP (Eastern Nile Council of Ministers) utakaofanyika tarehe 18 Agosti 2022; Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Bonde la Mto Nile (Nile Council of Ministers-NILECOM) pamoja na Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Ukanda wa Maziwa Makuu (Nile Equatorial Lakes Council of Ministers – NELCOM) itakayofanyika tarehe 19 Agosti 2022.
Akifafanua kuwa mikutano hiyo itatanguliwa na vikao vya Kamati za Wataalamu kutoka nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile (Nile Equatorial Lakes Technical Advisory Committee – NELTAC; Eastern Nile Technical Advisory Committee -ENTAC; na Nile Technical Advisory Committee – NILETAC).
Katibu Mkuu Sanga amesema mikutano hiyo inalenga kuendeleza ushirikiano wa Nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile katika kusimamia, kuendeleza na kutumia maji ya Mto Nile kupitia mipango, mikakati na programu za bonde la mto Nile kama vile Mpango Mkakati wa Bonde la Mto Nile (Nile Basin Strategy 2017-2027) na Programu ya Miaka Mitano ya Bonde la Mto Nile (5-Year Basin-Wide Program).

Aidha, Mhandisi Sanga amesema kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kupewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mikutano hiyo, itapokea uenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Bonde la Mto Nile kwa mwaka 2022/2023 kutoka nchi ya Jamhuri ya Sudan Kusini.
Hafla ya ufunguzi wa mikutano hiyo itafanyika tarehe 19 Agosti, 2022 kuanzia saa 02:00 asubuhi.
Bonde la Mto Nile, pamoja na Tanzania, linahusisha nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Misri, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Sudan na Uganda. Nchi hizo zinashirikiana katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji za Bonde la Mto Nile chini ya mwavuli wa Taasisi ya Mpito ya Nile Basin Initiative (NBI).

Ili kutekeleza dira ya pamoja, nchi za Bonde la Mto Nile zilianzisha programu katika Ukanda wa Maziwa Makuu kwenye Mto White Nile (Nile Equatorial Lakes Subsidiary Action Program – NELSAP) na katika Ukanda wa Mashariki kwenye Mto Blue Nile (Eastern Nile Subsidiary Action Program – ENSAP), Tanzania ikiwa katika Programu ya Ukanda wa Maziwa Makuu (NELSAP).