MAKAMU WA RAIS CRDB MARATHON

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewaasa watanzania kufanya utaratibu wa kufanya mazoezi kuwa  wa kudumu kwa kila mmoja ili kujiepusha na maradhi na kujipunguzia gharama  za matibabu ya magonjwa yanayoweza kuepukika kwa kufanya mazoezi mara kwa mara.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na washiriki wa mbio za hisani za CRDB Bank Marathon maalum kwaajili ya kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo na wakina mama wenye ujauzito hatarishi zilizofanyika Jijini Dar es salaam leo tarehe 14 Agosti 2022.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa kuhitimisha mbio maalum kwaajili ya kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo na wakina mama wenye ujauzito hatarishi za CRDB Bank Marathon zilizofanyika Jijini Dar es salaam leo tarehe 14 Agosti 2022. Amesema watanzania wengi, hususan wanaoishi maeneo ya mijini, wanakabiliwa na hali ya uzito uliozidi inayopelekea vifo kutokana na  magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari na shinikizo la damu.

Halikadhalika Makamu wa Rais ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa  mstari wa mbele katika utoaji wa huduma za fedha na misaada ya kijamii ambapo mbali na kutengeneza fursa za ajira, biashara na ujasiriamali, kupitia mbio hizi za hisani, Benki hiyo  imeweza kutoa takriban Shilingi bilioni 1 kusaidia wananchi wa kipato cha chini kupata matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Pamoja na uanzishwaji wa kituo cha kisasa cha taarifa na huduma kwa wagonjwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa taasisi nyingine za kifedha na wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi za serikali hasa katika kuhamasisha, kukuza uelewa na kujenga uwezo wa jamii na taasisi mbalimbali katika kuhifadhi mazingira. Amesema Serikali inaendelea na kampeni kote nchini kujanisha na kupendezesha miji hivyo kuunga mkono kutasaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na pia kutekeleza mikataba ya kimataifa kama Mkataba wa Kyoto (Kyoto Protocol) 2005; na Mkataba wa Paris (Paris Agreement, 2015).

Pia Makamu wa Rais ametoa wito kwa wadau na taasisi kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Watoto Njiti). Amesema wakati Serikali inaendelea kuboresha na kuimarisha huduma za watoto njiti, bado kuna vituo  vya kutolea huduma za afya vina upungufu wa vifaa tiba vya kusaidia watoto hao pamoja na kukosekana kwa elimu ya afya ya uzazi husasani katika maeneo ya vijijini.

Kwa upande Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema Benki hiyo inatambua wajibu ilionao katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya watanzania na hivyo kushirikiana na serikali na  kuwekeza katika masuala ya jamii ikiwemo afya, elimu, mazingira na uwekezaji kwa wanawake na vijana.

Amesema mafanikio yaliopatikana katika mbio hizo mwaka 2020 yalipelekea mbio za Benki ya CRDB kutambulika kimataifa na shirikisho la kimataifa la mchezo wa riadha ambayo imetoa heshima kwa taifa.

Mbio hizo zimeshirikisha Viongozi mbalimbali akiwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete, Naibu Spika wa Bunge Mheshimiwa Mussa Zungu, Mke wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango, Waziri wa Habari , Vijana ,Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Tabia Mwita Maulid,Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mheshimiwa Pauline Gekuli, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, viongozi wa kampuni na taasisi mbalimbali pamoja na wananchi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiongoza mbio za hisani za CRDB Bank Marathon maalum kwaajili ya kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo na wakina mama wenye ujauzito hatarishi zilizofanyika Jijini Dar es salaam leo tarehe 14 Agosti 2022.(Kushoto ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete Naibu Spika wa Bunge Mheshimiwa Mussa Zungu pamoja na Mkurugenzi Mtendaji CRDB Bank Abdulmajid Nsekela. Kulia ni Mke wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango pamoja na Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mheshimiwa Pauline Gekuli).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *