Mtendaji Mkuu wa TARURA Eng. Victor Seff amesema kuanzia mwaka 2021/22 hadi 2026/27 lengo ni kuongeza mtandao wa barabara za lami kwa km 1,450.75 kutoka km 2,404.90 zilizopo hivi hadi kufukia Km 3,855.65, changarawe km 73,241.57 kutoka km 29,116.57 hadi kufikia km 102,358.14 na madaraja 3,808 kutoka 2,812 hadi kufikia madaraja 6,620.

Aidha amebainisha kuwa fedha zitakazotumika kwenye mpango huu zinakadiriwa kuwa zaidi ya Shilingi trilioni 4.2.
Eng. Seff ameyasema hayo kwenye hafla ya Utiaji Saini Mikataba baina ya Wakandarasi wa Ujenzi wa Miundombinu ya barabara zinazosimamiwa na TARURA kwa mwaka wa Fedha 2022/23 uliofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center mapema leo Tarehe 14.08.2022 na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

‘Mpango Mkakati wetu wa pili ni kuwa ifikapo 2026/27 asilimia 85 ya mtandao wa barabara za Wilaya chini ya TARURA zitakuwa zinapitika kwa misimu yote na nyakati za mvua hapatakuwa na taharuki inayojitokeza sasa kwa maeneo mengi kujifunga.
Hii pia ina akisi kauli mbiu yetu ya Mpango Mkakati wa pili inayosema
TARURA TUNAKUFUNGULIA BARABARA KUFIKA KUSIKOFIKIKA’ alisisitiza Eng. Seff
Aliongeza kuwa Katika utekelezaji wa bajeti ya Mwaka 2022/23 jumla ya zabuni 1,706 zitatangazwa zenye thamani ya Shilingi 621.66 zilipangwa kutangazwa. Kwa awamu ya kwanza tulitangaza asilimia 60 ya bajeti sawa na zabuni 1,085 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 378.56, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo toka Ofisi yako TAMISEMI ya kufanya ununuzi wa asilimia 60 ya bajeti ili kazi zianze mapema kabla ya msimu wa mvua kuanza na pia tumeanza utekelezaji wa awamu ya asilimia 40 iliyobaki.
Kati ya zabuni 1,085 zilizotangazwa katika awamu ya kwanza, leo utashuhudia uwekaji wa saini mikataba 968 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 331.39. Zabuni nyingine zipatazo 117 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 47.17 zimerudiwa kutangazwa kutokana na kukosekana kwa Makandarasi wenye sifa maeneo hayo.
Jukumu kubwa la TARURA ni kusimamia Ujenzi/Ukarabati na matengenezo ya mtandao wa barabara za Wilaya wenye jumla ya kilomita 144,429.77. Kati ya urefu huo, kilomita 2,635.75 (1.82%) ni barabara za lami, kilomita 32,504.26 (22.5%) ni barabara za Changarawe na kilomita 109,289.77 (75.67%) ni barabara za udongo.
Pia kuna jumla ya Madaraja 3,191 na Makalavati 69,317 Hali ya mtandao wa barabara za Wilaya hadi kufikia Juni 2022; asilimia 23.6 (km 34,056) una hali nzuri, asilimia 33.7 (km 48,684.36) una hali ya wastani na asilimia 42.7 (km 61,689.42) una hali mbaya.
Kama takwimu zinavyoonesha, asilimia 75.67 ya mtandao wa barabara za Wilaya ni za udongo na zinaathirika sana wakati wa misimu ya mvua na kusababisha maeneo mengi kutopitika.

MATUKIO YA PICHA KATIKA HAFLA YA KUSAINI MIKATABA KATI YA TARURA NA MAKANDARASI







