Tumieni fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi – Mhandisi Zena

NA MWANDISHI WETU
VIJANA nchini wametakiwa kutumia fursa zinazowazunguka ili kujikwamua na
changamoto mbali mbali zinazowakabili.
Akifungua mdahalo Mdahalo wa Kijana Imara Transformative, ulioandaliwa na shirika la
Kiona Youth Coordinates (KYCo), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa
ya vijana inayoadhimishwa Agosti 12 ya kila mwaka, uliofanyika katika hoteli ya Golden
Tulip Zanzibar, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi
Zena Ahmed Said, amesema kufanya hivyo kutaongeza mchango wao katika taifa.
Ameeleza kuwa vijana wa Zanzibar na Tanzania kwa ujuumla wanakabiliwa na
changamoto mbali mbali lakini wakitumia vyema mipango na mikakati ya kitaifa na
kimataifa, watanufaika na kujikwambua katika lindi la umasikini.
Aidha alipongeza ushiriki wa AZAKI za vijana katika kubadilisha mitazamo na maisha
ya vijana nchini jambo linalosaidia juhudi za serikali katika utatuzi wa changamoto
zinazowakabili vijana.
Aliongeza kuwa vijana ni kundi kubwa katika jamii hivyo kuna umuhimu wa
kuunganishwa kwa mawazo na nguvu zao ili kuepuka kupeleka nguvu zao katika
mambo yasiyo na tija kwa taifa.
“Kwa kuzingatia kuwa vijana ni kundi kubwa hivyo kama hatutokua na njia nzuri ya
kutumia ‘energy’ (nguvu) hizo, wataipeleka mahali ambapo sio sahihi na matokeo yake
tunaweza kuharibikiwa kama taifa,” alieleza Mhandisi Zena.
Aidha alilipongeza shirika la KYCo kwa utekelezaji mzuri wa mradi wa ‘Kijana Imara’
unaolenga kuwawezesha vijana kubadilisha mitazamo yao kwani kufanya hivyo
kutawanya waelekeze nguvu zao katika uzalishaji mali.
Akizungumza wakati wa mdahalo huo uliohudhuriwa na vijana zaidi ya 250 kutoka
taasisi mbali mbali za vijana na Mabaraza ya vijana ya wilaya za Unguja, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fatma Hamad Rajab, alieleza
kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuratibu na kusimamia mipango ya
maendeleo ya vijana hivyo alipongeza mchango wa sekta binafsi kusaidia vijana.
Alisema vijana wana haki ya kutumia fursa zilizopo kujiimarisha kiuchumi na kupaza
sauti zao ili kupiga hatua za kimaendeleo na kwamba wizara yake itaendelea kutoa kila
aina ushirikiano kwa asasi za vijana na wadau wa maendeleo kufikia malengo ya vijana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *