TANROADS WAASWA KUWA WABUNIFU KUPUNGUZA GHARAMA ZA UJENZI

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), wameaswa kuwa wabunifu na
mstari wa mbele katika ulindaji wa miundombinu inayojengwa kwa gharama
kubwa na Serikali pamoja na kutumia malighafi zinazopatina sehemu husika ili
kupunguza gharama zinazotumika katika ujenzi wa miundombinu ya barabara,
madaraja na mizani hapa nchini.
Agizo hilo limetolewa mkoani Njombe na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na
Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Balozi Mhandisi Aisha Amour, katika kikao kazi na
watumishi wa Wakala huo ambapo amesisitiza weledi, ubunifu, matumizi ya
kisasa ya TEHAMA ili kuleta ufanisi katika utendaji wao kazi.
“Nahitaji mabadiliko kwa watumishi wa TANROADS katika matumizi ya teknolojia
maana huko kuna vitu vingi vya kujifunza badala ya kupoteza muda kuangalia
masuala yasiyokuwa na tija katika utendaji kazi wenu”, amesisitiza Balozi Aisha.
Ameongeza kuwa Wizara imepanga kutoa motisha kwa watumishi ambao
watakuja na mawazo mapya yenye kuleta tija katika uboreshaji na usimamizi wa
miundombinu iliyopo na inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.
“Hakikisheni mnaibua vipaji vya watumishi wenu mahala pa kazi kwa kuhakikisha
kila mtumishi aliyeajiriwa anatekeleza majukumu yake ipasavyo na kuondoa
dhana ya watu wachache kuonekana bora zaidi”, amesema Katibu Mkuu huyo.
Awali akitoa taarifa ya mkoa huo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS), mkoa wa Njombe Mhandisi Kipembawe Msekwa ameeleza kuwa
ujenzi wa barabara ya Njombe – Makete na Itoni – Ludewa – Manda
zinazounganisha Makao Makuu ya Mkoa na Wilaya (Ludewa na Makete) tayari
zimeanza kutoa matunda katika shughuli za usafiri na usafirishaji wa abiria na
mazao kutoka shambani na kukuza uchumi wa mkoa.
“Barabara hizi zimepelekea muda wa safari kupungua hadi wastani wa saa mbili
(kutoka Makete) na saa tatu (kutoka Ludewa) ambapo hapo awali hasa kipindi
cha masika muda wa safari ulikuwa ni mwendo wa siku nzima”, amefafanua
Mhandisi Msekwa.
Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Njombe unahudumia
matengenezo ya barabara yenye jumla ya (km 1,188.23) kati ya hizo (km
403.420) ni Barabara Kuu na (km 784.810) ni Barabara za Mkoa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Balozi Mhandisi Aisha
Amour, akizungumza na watumishi wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa
Njombe (hawapo pichani), wakati walipofanya kikao kazi na watumishi hao kuhusu
uboreshaji wa utendaji kazi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *