NHC yaombwa kuifikia mikoa ya pembezoni

WANANCHI wameliomba Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) kujenga nyumba na kuweza kuifikia mikoa mbalimbali ya pembezoni kwa lengo la kutatua changamoto ya nyumba na makazi kwa watumishi na wananchi wa maeneo hayo.

Wananchi hao wameyasema hayo leo kwa nyakati tofauti baada ya kutembelea banda la shirika hilo katika maonyesho ya wakulima Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nanenane, John Mwakangale mkoani Mbeya.

Aidha NHC wametakiwa kuongeza nguvu kuhakikisha wanafanya uwekezaji katika mikoa hiyo ili kupunguza adha kwa wananchi wenye uhitaji nauwezo wa kununua na hata watumishi wa umma kupata nyumba bora na za kisasa kwa ajali ya kupanga.

‘’Tumeona na kusikia Shirika la Nyumba la Taifa likijenga nyumba katika maeneo ya mijini Kama Dar es Salaam kule Kawe, Kibada na hata kule Morocco Square… Mzee wangu aliniuliza kwanini na sisi huku mikoani hawatujengei,”amesema Amelita Mambo Mkazi wa Mbeya.

Amelitaka Shirika liangalie hii mikoa iliyo pembezoni zipatikane nyumba za kuishi Watanzania, wengine wanakata tamaa ya kazi kutokana na ukosefu wa makazi.

Naye Oddo Hekela akizungumza kwenye maonyesho hayo amesema kuwa amevutiwa na riba ndogo inayotolewa na Benki ya Azania katika utoaji wa mikopo ya nyumba na amesema kwamba hiyo itakuwa mkombozi kwa Watanzania wengi wenye nia ya kununua nyumba kwa mikopo kwani itawapa unafuu wa maisha.

Akijibu matarajio hayo ya wananchi, Ofisa Mkuu wa Mauzo na Masoko wa Shirika la Nyumba la Taifa, Emmanuel J. Lyimo amesema kuwa Shirika linaendelea na ujenzi wa nyumba za makazi katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kufikia lengo hilo na kwamba hivi karibuni litaanza ujenzi wa nyumba 400 katika eneo la Kawe kwa ajili ya wananchi wa kipato cha kati cha chini.

Maonesho hayo ya Nane Nane yamefunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 1 Agosti 2022 yanafanyika katika Uwanja wa John Mwakangale Jijini Mbeya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *