
OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa amemuagiza mkandarasi wa daraja la Berega kumaliza kazi kwa wakati ili kuwaondolea adha wananchi wa Kilosa, Gairo, Kiteto na Kilindi wanaotumia daraja hilo kusafirishia mazao yao haswa wakati wa mavuno.
Daraja hilo la zege lenye urefu wa mita 140 na upana wa mita 11 linaunganisha Wilaya za Kilosa, Gairo na Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga na linajengwa kwa thamani ya Sh bilioni 7.9.
Bashungwa alitoa agizo hilo mara baada ya kukagua ujenzi wa daraja hilo ambalo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 13.7.

Alisema hataki visingizo na kumtaka mkandarasi kuhakikisha anakamilisha daraja hilo kwa wakati uliopangwa.
” Sitaki kusikia sababu kuwa mvua zimekwamisha ujenzi, kipindi hiki ni kiangazi, sasa hakikisheni mnafanya kazi mchana na usiku ili mkamilishe kwa wakati.”
Naye Mbunge wa Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za Kujenga daraja hilo ambalo ni muhimu Kwa wananchi na kuwa litachochea uchumi.
Alisema Serikali ya Rais Samia imetoa fedha nyingi za kuboresha miundombinu ya barabara, kujenga makaravati makubwa, miundombinu ya elimu na afya.

Kazi zingine zitakazofanyika sambamba na ujenzi wa daraja hili ni ujenzi wa barabara zinazounganisha daraja hili, ujenzi wa barabara kutoka Berega barabara mpaka darajani kwa kiwango cha changarawe, nyumba za wakandarasi pamoja Ofisi ambazo baada ya kazi zitakabidhiwa kwa Mkurugenzi pamoja na kazi nyinginezo.
