UHUSIANO MZURI KATI YA NCHI ZA TANZANIA NA MAREKANI WAONGEZA IDADI YA WATALII NCHINI


  • Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi ya Marekani umesaidia kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania.

Ameyasema hayo leo Julai 23,2022 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati wa mapokezi wa Watalii 60 kutoka nchini Marekani.

“Marekani ni miongoni mwa masoko yetu ya utalii ya kimkakati yaliyoanza kuonesha matumaini makubwa katika kuirejesha Sekta ya Utalii baada ya kuathirika na Janga la UVIKO-19 kwa mfano mwaka 2021 tulipokea watalii 48,537 kutoka nchini humo sawa na ongezeko la asilimia 55 ikilinganishwa na watalii 31,211 kwa mwaka 2020” amefafanua Mhe. Masanja.

Aidha, ameweka bayana kuwa ongezeko hilo la idadi ya watalii ni kutokana na Programu Maalum ya kimkakati ya Tanzania-The Royal Tour iliyoasisiwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema tangu kutangazwa kwa Royal Tour idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma.

“Katika kipindi cha mwezi Januari hadi Mei, 2022 idadi ya watalii waliotembelea Tanzania ilifikia watalii 458,048 sawa na ongezeko la asilimia 44.4 ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka 2021 ambapo tulipokea watalii 317,270”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *