Serikali yaboresha miundombinu ya viwanja vya michezo mashuleni

Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo kwa kuendelea kutoa fedha kujenga na kuboresha viwanja katika shule za Msingi na Sekondari ikiwa ni kutambua umuhimu wa somo la michezo na kuendelea kuibua vipaji kwa wanafunzi.

Hayo ameyasema Julai 21, 2022 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Batilda Burian wakati akikagua viwanja vinavyoendelea kujengwa na vinavyoendelea kufanyiwa ukarabati katika Shule ya Sekondari ya wavulana Tabora na Shule ya Wasichana Tabora ikiwa ni maandalizi ya michezo ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule ya Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Mashindano ya Umoja wa Michezo Sekondari Tanzania (UMISETA).

Dkt. Batilda amesema, pamoja na maendeleo mazuri yanayoendelea katika ujenzi huo amewataka wasimamizi na mafundi kuzingatia muda, ubora na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali katika uwekezaji wa ujenzi wa viwanja hivyo na kusema si tu vitatumika kwa michezo hiyo bali ni viwanja endelevu vitakavyoendelea kutumika kizazi hadi kizazi.

“Ninamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya michezo, sisi viongozi tutaendelea kusimamia miradi yote ya maendeleo inayoletwa na Serikali ili kuhakikisha inajengwa kwa ubora na kukamilika kwa wakati” amesema Dkt. Batilda

Kuhusu Maandalizi ya mashindano ya Michezo ya UMISETA na UMISHUMTA yatakayofanyika Kitaifa Mkoani Tabora amesema, Mkoa umejipanga kupokea wageni wote na kuwahakikishia uwepo wa mahitaji muhimu yatakayohitajika na kuahidi kutoa ushirikiano na wapo tayari kupokea mashindano hayo.

“Nitoe wito kwa wenyeji wenzangu tufanye kazi kwa kujituma na kwa amani ugeni huu utatusaidia kuongeza kipato endapo tu tutajituma kwa kufanya biashara zetu za kihalali na amani tuboreshe biashara kama mnavyofahamu Tabora hatuna jambo dogo” amesisitiza Dkt. Batilda

Kwa upande wa Afisa Elimu Mkoa Mwl. Juma Kaponda ameishukuru Serikali kwa kupendekeza mashindano hayo kufanyika Mkoa huo na kuwataka washiriki wenyeji kuwa tayari kushiriki na tayari wanajinoa kwa kuendelea kufanya mazoezi.

Naye Mratibu wa Michezo Ofisi ya Rais – TAMISEMI Bw. George Mbijima amesema, maandalizi yapo vizuri na yamekamilika na washiriki 3900 watashiriki michezo ya UMITASHUMTA na washiriki 4200 UMISETA ambapo itahusisha na viongozi wa michezo hiyo.

Aidha, ametoa wito kwa washiriki wa michezo kuonesha vipaji vyao kwa kuzingatia sheria na taratibu za michezo kutoka kwa walimu kwani michezo ina sheria zake kama ilivyo katika masomo mengine.

Mashindano ya michezo ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule ya Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Mashindano ya Umoja wa Michezo Sekondari Tanzania (UMISETA) inashirikisha Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *