TMA YATOA UFAFANUZI MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA KATIKA MAENEO YA UKANDA WA PWANI.

Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam.

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imewataka wadau mbalimbali kuendelea kuchukua tahadhari kuhusu na ushauri na utabíri unaotolewa na TMA ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza.

Akizungumza jijini Dar es Salaam  Mtaalamu na Mchambuzi wa Hali ya Hewa, Kitengo kikuu cha Utabiti Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Bi. Rose Senyagwa, amesema kuwa mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo ya nyanda za juu Kaskazini Mashariki zimesababishwa na upepo wenye unyevuunyevu unaovuma kutoka bahari ya hindi kueleka katika maeneo ya nchi yetu.

Amesema kuwa mvua hizo zinasukumwa  na unyeunyevu ambapo zinaendelea kunyesha katika maeneo ya ukanda wa Pwani katika Mikoa ya Tanga, Dar es salaam, Pwani, Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, lindi, Mtwara,Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na baadhi ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

“Mvua hizi zilianza mwezi Juni mwaka huu  katika kipindi cha Kipupwe na zimekuwa zikijitokeza kwa mvua za kawaida, hivyo wameziita mvua za nje ya msimu na zinatarajia zitaendelea kuwepo katika kipindi cha Mwezi July mpaka Agosti mwaka huu” amesema 

Amesema kuwa kutokana na utabiri wa msimu wa kipupwe ambao ulitolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa mwishoni mwa mwezi Mei maeneo mengi ya nchi yalitarajiwa kuwa na vipindi vya baridi na upepo mkali.

Amesema katika maeneo ya ukanda wa Pwani na Maziwa Makuu vipindi vya upepo mkali bado vinatarajiwa kuendelea kujitokeza upepo unaofikia Kilomita 40 au kuzidi kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofika mita mbili yanatarajiwa kuendelea kujitokeza

Amebainisha kuwa ni vyema katika kipindi hicho cha baridi na upepo mkali wananchi wakazingatia tahadhari zinazotolewa kwa kujikinga ili kujihadhari na madhara ya kiafya.

TMA imetoa wito kwa washauri na wananchi wanaofanya shughuli zao kuendelea kuchukua tahadhari katika kipindi cha upepo mkali ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *