SERIKALI YAENDENDELEA KUBORESHA UTENDAJI WA TMA.

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imesema itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya Hali ya Hewa nchini ili kuongeza usahihi wa utoaji wa taarifa za Hali ya Hewa kwa wadau wote wakiwemo usafiri wa Anga, Ulinzi, Uvuvi na Usafiri wa Nchi Kavu.

Akizungumza mara baada ya kutembelea rada ya hewa iliyojengwa mkoani Mtwara, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amesema uhakika wa utabiri utachangia umakini katika uendelezaji wa miundombinu nchini katika nyanja zote.

“Nawapongeza sana kwa kukamilisha mradi huu na nichukue fursa hii kuwambia wananchi kuwa Serikali tayari iko kwenye hatua mbalimbali za kuongeza rada kufikia saba ili kuhakikisha usahihi wa utabiri unaongezeka”, amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amesema kuwa pamoja na uwezekezaji huo amewataka Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) kuhakikisha inabuni njia mbalimbali za kutoa taarifa ili kuwafikia wadau wote kwa wakati na kurahisisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Naye, Mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga, ameiomba Wizara kuijenga barabara inayoingia kwenye miudombinu kuijenga kwa kiwango cha lami kwani barabara hiyo inapata changamoto hasa nyakati za mvua.

“Mhe Naibu Waziri Wizara hii ina fedha hebu tizame kwenye bajeti angalau kilomita hizi chache mziwekee lami ili kulinda miundombinu hii mliyoijenga kwa fedha nyingi’ amesisitiza Mbunge Mtenga.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miundombinu wa TMA, Dkt Paschal Waniha, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya hali ya hewa na kusema kuwa uwepo wa rada hizo umeanza kuleta mabadiliko hasa kwa wadau wa Mikoa ya Kusini.

Kuhusu utabiri kuwafikia wadau, Dkt. Waniha amesema TMA inatumia njia za ujumbe mfupi (sms), mitandao ya kijamii, maonesho mbalimbali ya kitaifa na kutumia vyombo mbalimbali vya habari lengo likiwa kuwaafikishia taarifa sahihi na kwa wakati.

Naibu Waziri Mwakibete yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya siku tatu kukagua miundombinu inayojengwa na Wizara mkoani humo.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete (kulia) akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya
Mtwara, Dunstan Kyobya kuhusu miradi mbalimbali iliyopo mkoani hapo, wakati Naibu
Waziri huyo alipotembelea Ofisi za Mkoa wa Mtwara.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akizungumza na Wabunge, Viongozi wa
Mkoa na Watendaji wa Taasisi za Wizara Mkoani Mtwara wakati wa ziara yake mkoani
humo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete (katikati) katika picha ya pamoja na
Wabunge Viongozi wa Mkoa wa Mtwara na Watendaji wa Taasisi za Wizara wakati wa ziara
yake mkoani humo.

Muonekano wa rada ya hali ya hewa iliyojengwa katika eneo la Mbae Juu mkoani Mtwara.
Uwepo wa rada umeongeza uhakika wa utabiri wa muda mfupi na mrefu hususani katika
mikoa ya Kusini mwa Tanzania.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akisisitiza jambo mara baada ya kukagua
rada ya hali ya hewa iliyojengwa katika eneo la Mbae Juu mkoani Mtwara. Kulia ni Mkuu wa
Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya na Kushoto ni Mkurugenzi wa Miundombinu wa
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Paschal Waniha.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akimsikiliza Mkurugenzi wa Miundombinu
wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Paschal Waniha (kushoto) kuhusu
utendaji wa rada ya hali hewa iliyojengwa katika eneo la Mbae Juu mkoani Mtwara. Kulia ni
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya.

(Imetolewa na Kitengo cha Mawasilian Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *