
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete amempa Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wiki mbili kuhakikisha
analeta watumishi wa kudumu katika Bandari ya Lindi ili kurahisisiha
usafirishaji wa abiria na mizigo katika Bandari hiyo.

Akizungumza mkoani Lindi mara baada ya kutembelea Bandari hiyo Naibu
Waziri Mwakibete pamoja na maelekezo hayo amesisitiza umuhimu wa Bandari
kufanya vikao na wadau wote ili kuwa na mkakati wa pamoja wa namna ya
kuifanya bandari hiyo kurejea katika ufanisi kama awali.
“Bandari hii naelezwa ilikuwa inahudumia mzigo mkubwa sana miaka ya
nyuma lakini kwa sasa inaonekana imepoa sana na hakuna mzigo
unaosafirishwa hapa wakati gharama za mzigo kwa kusafirisha kwenye maji ni
rahisi kuliko kuupitisha barabarani”, amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete ameeleza kuwa kwa sasa Serikali imeamua
kupunguza tozo kwa asilimia 30 kwa mizigo inayosafirishwa kupitia Bandari za
Mtwara na Lindi ili kuruhusu mzigo mkubwa kupita bandarini ili kuongeza
ufanisi kwa utendaji wa Bandari hizo.

Naye, Mbunge wa Lindi Mjini, Hamida Abdallah, ameiomba Serikali
kuiboresha Bandari hiyo kwani hapo awali ilikuwa ni eneo ambalo lilitoa ajira
na kukuza pato la mkoa kwa usafirishaji mkubwa wa bidhaa za mbalimbali
ikiwemo mbao na saruji.

“Mhe Naibu Waziri Bandari hii ilikuwa inasafirisha mizigo na ilifika mahala
mpaka meli za Zanzibar zilikuwa zinakuja hapa kuchukua mizigo lakini kwa
sasa tunapokea meli ndogondogo ambazo zinabeba mzigo mdogo na kufanya
ufanisi usionekane”, amefafanua Mhe. Hamida.

Awali akitoa taarifa ya Bandari, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Abdilah Salim,
amesema miongoni mwa juhudi zinazofanywa na TPA kwa sasa ni kuendelea
na kufanya upembuzi yakinifu lengo likiwa ni kuboresha miundombinu ya
kibandari, vyombo vya kuhudumia shehena na meli ili kuruhusu bandari
kufanya kazi wakati wote.
Bandari ya Lindi kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imehudumia shehena ya tani
zaidi ya 8,574 ambazo zinajumuisha mizigo mbalimbali ikiwemo mazao ya miti
pamoja na bidhaa nyingine.

(Imetolewa kitengo cha Mawasiliano Serikali, WIzara ya Ujenzi na Uchukuzi)