
OR TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa ametoa onyo kali kwa wataalamu na watumishi walio chini ya Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa wanaoingilia na kujihusisha na masuala ya siasa katika wilaya ya Temeke mkoani Dar es salaam.
Bashungwa ametoa onyo hilo Jalai 08, 2022 alipokiwa akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Temeke na kukemea hali hiyo inayoendelea katika baadhi ya wilaya nchini na kueleza kuwa jambo hilo linafuatiliwa kwa ukaribu na wahusika watachukuliwa hatua za kinidhamu.

“Tunahitaji utulivu na kujenga umoja na mshikamano wa viongozi katika Wilaya ya Temeke ili utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi uweze kufanyika kwa ufanisi na weledi mkubwa, lakini kuna baadhi ya wataalam wachache wanaingilia masuala ya siasa, jambo hili nalikemea,” amesema Bahungwa

Bashungwa amewataka watumishi na wataalamu kujikita katika majukumu yao na kuacha masuala ya siasa yakafanywe na wanasiasa na vyama vyao kwa mjibu wa sheria na taratubu za nchi zinavyoelekeza.
Amesema anataka kusikia umoja na mshikamano katika wilaya hiyo na kuondokana na masuala ya mitengano na migawanyiko inayotokana baadhi ya watu kuilingilia masuala ambayo yapo nje ya mipaka yao ya utawala wao.

Aidha, Bashungwa amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Elihuruma Mabelya kuhakikisha ndani ya kipindi hiki cha kufunga hesabu za mwaka wa fedha 2021/ 22 kuhakikisha hoja za ukaguzi haziibuki.
” Sitarajii kuona hoja mpya za CAG zinaibuliwa na unatakiwa kujifunza katika mapungufu yaliyojitokeza miaka ya nyuma ili kuepuka hoja mpya kwa mwaka wa fedha ulioanza.”
Pia, amemtaka Meya wa Manispaa ya Temeke pamoja na Madiwani kushirikiana na Mkurugenzi kusimamia vizuri fedha za miradi ya maendeleo za mwaka wa fedha ulioisha na zinazoendelea kutumika na kutekeleza miradi katika mwaka huu wa fedha wa 2022/23.