
ROMBO JULAI 8, 2022
Waziri wa Ardhi Nyumba na Madndeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameipa mwezi mmoja Halmashauri ya wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro kuhakikisha inatekekeza mradi wa kupima, kupanga na kumilikisha ardhi kufikia julai 31, 2022 vinginevyo kiasi cha shilingi milioni 700 kati ya bilioni 1.060 ilizopewa kwa ajili ya mradi huo zitahamishiwa halmashauri nyingine za mkoa huo.
Hatua ya Dkt Mabula inafuatia Halmshauri hiyo kushindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati ambapo hadi sasa imefanikiwa kutumia shilingi milioni 60 tu kati ya bilioni 1.060 ilizopewa kwa ajili ya kutekeleza mradi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halmashauri ya wilaya ya Rombo inaonesha kama haistahili kupata fedha za mradi huo pamoja na kuwa na andiko zuri la kupatiwa fedha kwa ajili ya utekekezaji wa mradi huo.
Halmashauri ya wilaya ya Rombo iliomba shilingi Bilioni 1.060 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika eneo la Holili hisusan kitongoji cha Holili shuleni ambapo uchaguzi wa eneo hilo ulizingatia eneo lisilokuwa na maendelezo mengi kuepuka ukuaji holela wa mji.

