MCHECHU AENDELEA KUUPIGA MWINGI, ASISITIZA KUAMSHA UTEKELEZAJI SERA YA UBIA

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Nehemiah Kyando Mchechu amekutana na Uongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwaelezea mipango ya Shirika na sekta ya nyumba inayotarajiwa kutekelezwa na NHC kuanzia Agosti 2022 ikiwemo utekelezaji wa sera ya ubia na sekta binafsi
Katika Mkutano wake huo kwa Viongozi wa Wizara hiyo wakiongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, leo tarehe 8/7/2022 Kambarage House Jijini Dar es Salaam, Bw. Mchechu amesema Shirika hivi sasa limejikita katika kuanza miradi hiyo ya kimkakati kwa kasi na ari kubwa.
Katika maelezo yake Mkurugenzi Mkuu alielezea miradi ya ujenzi itakayotekelezwa kuwa ni pamoja na mradi wa nyumba 5,000 utakaotekelezwa kwa awamu tatu tofauti.
Kuhusu Sera ya Ubia amesema sera hiyo itashirikisha sekta binafsi ili kuongeza kasi ya kuwapatia Watanzania nyumba nyingi na bora.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu alielezea uongozi huo kuwa ili kuweza kusukuma mbele ajenda ya nyumba nchini, Shirika linahitaji rasilimali watu makini ambayo italiwezesha kupata tija na kujibu matarajiyo ya watanzania kwa haraka.
Akizungumza baada ya kuwasilishwa kwa Mpango huo, Waziri Mabula amepongeza mikakati yake mikubwa ya ujenzi wa nyumba ambazo zitawanufaisha Wengi zaidi kuiomarisha uchumi wa Shirika na wa Taifa kwa ujumla.
Amesema Wizara yake italiunga mkono Shirika la Nyumba la Taifa katika kufanikisha ndoto zake za kuwapàtia watanzania makazi bora na ameikaribisha Menejimenti ya Shirika kuleta mapendekezo yoyote itakayoona yanafaa kujadiliwa na pande zote ili kuliwezesha Shirika kufanikisha Mipango yake iliyojiwekea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *