MC PILIPILI ACHUKUA FOMU KUWANIA UONGOZI CCM

Kufuatia tangazo lililotolewa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Dodoma kwa wanachama wote kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama aliyewahi kuwa mgombea ubunge jimbo la Dodoma Mjini Robert Mtyani pamoja na Emmanuel Mathias alimaarufu MC Pilipili wamejitokeza kama vijana kuchukua fomu za kuwania nafasi hizo.

Robert Mtyani amechukua fomu ya kugombea nafasi ya Katibu wa siasa na uenezi Mkoa ambapo amesema ameamua kujitokeza kuwania nafasi hiyo akiamini kwamba amepikwa kupitia nafasi mbalimbali ambazo amewahi kuzitumikia katika chama hicho.

“Najiamini kwamba nimekuwa nikipikwa vizuri kupitia chama, na mimi nimeona mchango pekee wa kumsaidia mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mhe Rais Samia Suluhu Hassan ni kujitokeza kuomba nafasi hizi ili tuweze kukisaidia chama,na matarajio yangu ni kuhakikisha kwamba CCM inaendelea kuwa ni Chama ambacho kinaaminiwa na Watanzania.

Mtyani amesema ili chama kiendelee mbele Zaidi kinapaswa kuwa na viongozi wa kujitolea Zaidi na wenye maadili ili watanzania waendelee kupata maendeleo.

Naye Emmanuel Mathias (MC Pilipili) ambae yeye amechukua fomu ya kuwania Ujumbe wa Halmshauri kuu ya Taifa CCM amesema anaamini kuwa CCM ndio Chama kinachowapika viongozi ambao baadae wanakuja kushika Dola.

“Nafasi za kuwatumikia wananchi kila mtu anaweza akagombea lakini mimi nimekuja kuchukua fomu katika tawi langu la Kigwe nikiamini kwamba najiandaa kwenda kuwatumikia wananchi, na mimi ningependa kutoa shime kwa vijana wajitokeze katika kuwania nafasi hizi kwa maendeleo ya nchi yetu”amesema Pilipili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *