
Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Serikali imetoa maelekezo 11 kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa Sehemu za Mipango, Uratibu na Serikali za Mitaa, Maafisa Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji na Waweka Hazina wa Halmashauri wanayopaswa kuyatekeleza kwa tija na ubunifu ikiwemo la kusimamia mpango ya bajeti na kuongeza uwajibikaji wa pamoja.
Maelekezo hayo yametolewa leo tarehe 7 Juni, 2022 Jijini Dodoma na Naibu Katibu Ofisi ya Rais ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt. Grace Magembe (afya) aliyemwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikai za Mitaa, Innocent Bashungwa wakati wa kufungua kikao kazi cha siku mbili kwa maafisa hao.
Amesema kuna haja ya kuwa na uwajibikaji wa pamoja kwa watumishi wa Mikoa na Halmashauri sambamba na kusimamia utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/23.
“ Mikoa na Halmashauri ni taasisi ambazo kila kinachofanyika lazima kila mmoja ahakikishe amefanya kwa nafasi yake badala ya kuja na visingizio mimi sijui, mimi sikuhusika maana mwisho wa siku wote tutawajibika kwa utendaji mzuri au mbaya wa taasisi.” Amesisitiza Dkt. Magembe
Amewahimiza kusimamia kwa karibu ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za umma ikiwamo zile za mapato ya ndani ya halmashauri ili ziweze kutekeleza miradi iliyopangwa na Serikali .
“ Niendelee kukemea matumizi ya fedha mbichi na niwatake kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na kuchukua hatua kwa wakati kwa watendaji watakaoshindwa kutimiza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma na zile za taaluma zao.” amesema Dkt. Magembe
Pia awamataka maafisa hao kuhakikisha wanasimamia umalizaji wa miradi kwa wakati na viwango na kuwa serikali haitavumilia kuona kuna miradi viporo. Aidha, amewataka kusimamia na kuratibu upelekezaji wa asilimia 40 au 60 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwenye miradi ya maendeleo.
Dkt Magembe amewaeleza kuwa kuanzia sasa utendaji wa sekretariati za mikoa na mamlaka ya serikali za mitaa pamoja na mambo mengine utapimwa kwa vigezo vya upelekaji wa fedha za miradi asilimia 40 kwa 60 kwenye miradi ya maendeleo,pia kuhakikisha wanasimamia upelekaji, matumizi na urejeshwaji wa wa fedha za mikopo ya asilimia 10
Pia amesisitiza suala la matumizi na usimamizi wa mifumo ya ndani ya udhibiti wa makusanyo na matumizi ya fedha ili kuhakikisha hoja za ukaguzi zisijitokeze na kuhakikisha hoja za zamani zinajibiwa na kufungwa.
“ Hili suala la kutozalisha hoja mpya za ukaguzi na kuzimaliza zilizoibukwa pia kitatumika kama kigezo cha utendaji wenu hivyo tuache visingizio.”
Maofisa hao pia wametakiwa kusimamia uandaaji wa Taarifa ya Mwisho ya Hesabu za fedha Mamlaka za Serikali za mitaa kwa wakati na kwa usahihi na kusimamia usluhisho wa kifedha unafanyika kila mwisho wa mwezi kwa kuzingatia memoranda ya fedha za Serikali za mitaa ya mwaka 2009.
“ Hakikisheni mnafuatilia mara kwa mara wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizopo katika Mikoa unafanyia ili kuwa na thamani ya fedha kama ilivyokusudiwa.” amesisitiza
Aidha, amekumbusha kuwasilisha maombi ya fedha za miradi ya maendeleo kupitia ruzuku ya Serikali kuu mapema ili kuwezesha utekelezaji wa miradi iliyopangwa utekeleaji kuanza mapema.



