
Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph amesema wakazi wa Ntyuka-Chimala jijini Dodoma wameondokana na adha ya kufuata maji kwa umbali mrefu baada ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji uliotekelezwa kupitia fedha za Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Amesema Mradi huo umeghrimu takribani Sh.Milioni 471.8 ambapo fedha za UVIKO-19 zilikuwa Sh. Milioni 359.7 na Sh.Milioni 112 zimetolewa na Mamlaka hiyo kutoka kwenye vyanzo vyake vya mapato vya ndani,
ameyasema hayo jumanne Julai 5, 2022 katika ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma ilipotembelea na kukagua mradi wa maji Ntyuka Chimala.
Alisema wananchi wa eneo hilo walikuwa hawana kabisa huduma ya maji safi na hivyo kulazimika kutembea umbali wa kilometa tano hadi saba kufuata huduma ya maji maeneo mengine.
“Serikali kwa kutambua athari za ugonjwa wa UVIKO-19 imetenga fedha za utekelezaji wa mradi wa mfumo wa maji safi eneo la Ntyuka Chimala, Duwasa ilipokea Sh.Milioni 359.7 lakini hazikutosha kukamilisja mradi mpaka kufikisha maji kwa wananchi, hivyo kupitia makusanyo ya ndani tuliongeza Sh.Milioni 112,”alisema.

Mkurugenzi huyo alisema mradi umetekelezwa ndani ya miezi sita na utanufaisha wakazi wa eneo hilo 4,558.
“Upatikanaji wa maji kwasasa umetoka asilimia sifuri hadi 95, tunashukuru serikali kwa kutoa fedha kutekeleza miradi ya maji na kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji maeneo mbalimbali Dodoma,”alisema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Dodoma, Damas Mukasa, alitoa rai kwa wananchi kujitokeza kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa maji kwenye nyumba zao.
Aliwataka kutunza mradi huo ili udumu na kutoa huduma endelevu.
“Tunashukuru kanisa la Anglikana kwa kutoa eneo hili bure la huu mradi, sasa wananchi wenzangu tujiepushe na uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji, na hii miundombinu ni muhimu kuitunza ili mradi wetu udumu,”alisema.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri, alishukuru serikali kwa kuwatua ndoo kichwani akinamama waliokuwa wakipata adha kubwa ya maji kwa kutembea umbali mrefu na wakati mwingine kununua ndoo kwa Sh.100.
