GRAPHITE KUANZA KUCHIMBWA RUANGWA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali ipo katika majadiliano na kampuni ya Uranex kwa ajili ya ujenzi wa mgodi wa madini ya bunyu (graphite) utakaoanza hivi karibuni.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa wananchi wa wilaya ya Ruangwa wajiandae kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zitokanazo na ujenzi wa mgodi wa graphite.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Julai 5, 2022) wakati akizungumza na wananchi katika vijiji vya Namikulo, Namkatila na Matambarale katika kata ya Chunyu wilayani Ruangwa, Lindi.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kila kwenye rasilimali kabla ya kuanza uwekezaji lazima wahusika wajadiliane na Serikali ili kubaini namna ambavyo itanufaika.”

Waziri Mkuu amesema wakazi wa maeneo hayo watakuwa ndio wanufaika wa kwanza kutokana na shughuli mbalimbali zinakazokuwa zikiendelea kuanzia hatua ya ujenzi hadi uzalishaji.

“Kila shughuli itakayofanyika hapa ni fursa kwetu sisi wana-Namikulo na wana-Ruangwa kiujumla. Tujipange sawa sawa Serikali yenu ipo makini kuhakikisha mnanufaika na mradi huo.”

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa kampuni ya Uranex, Mhandisi Isaac Mamboleo amesema kampuni yao inatarajia kuanza ujenzi wa mgodi huo katika mwaka huu wa fedha.

Amesema mradi huo ambao utahusisha vijiji saba unatarajia kugharimu shilingi bilioni 625 na utazalisha ajira 950 kati yake ajira 600 wakati wa ujenzi na ajira 350 wakati wa uzalishaji.

Mhandisi Mamboleo amesema kwa sasa wanakamilisha ujenzi wa nyumba 59 zenye gharama ya shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kuwafidia baadhi ya wananchi waliopisha ujenzi wa mradi huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *