WAKAZI 17,000 KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI WA FEDHA ZA UVIKO-19

MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph amesema zaidi ya wananchi 17,000 katika maeneo ya Bahi mjini wilayani hapa mkoani Dodoma, wanatarajia kunufaika kupitia mradi wa maji unaotekelezwa kwa fedha za Maendeleo ya Ustawi na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Mradi huo unatarajia kuboresha upatikanaji maji katika mji wa Bahi kwa kuongeza lita 528,000 kwa siku sawa na ongezeko la asilimia 51.7 za lita 377,000 zinazozalishwa kwa siku.

Akizungumza wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ilipotembelea mradi huo juzi Julai 3, 2023, alisema ongezeko hilo litafanya uzalishaji kufikia lita 905,000 kwa siku sawa na asilimia 88.7.

“Serikali kwa kutambua athari za ugonjwa wa UVIKO-19 imetenga fedha za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mfumo wa maji safi eneo la Bahi. DUWASA ilipokea fedha sh. milioni 451.5 kutekeleza mradi huu.

Aliongeza kuwa: “Ili kukamilisha mradi huu na kufikisha maji kwa wananchi, DUWASA kupitia makusanyo yake ya ndani na vyanzo vingine iliongeza sh. milioni 67.4 kugharamia baadhi ya kazi ili kukamilisha mradi.”

Mhandisi Joseph alisema jumla ya gharama za kutekeleza mradi huo ni sh. milioni 515.1 ambazo zilitumika katika kazi mbalimbali za mradi.

Alizitaja kazi hizo ni utafiti wa maji chini ya ardhi kupata maeneo ya kuchimba visima, ujenzi wa tanki la ujazo wa lita 200,000, ulazaji mabomba ya kupeleka maji katika tenki na mabomba ya kusambazia maji yenye kipenyo vya kati ya 50mm na 160mm, ununuzi na usimikaji pampu za kuzalisha maji.

Pia, alisema kazi nyingine zilizohusisha mradi huo ni ununuzi na usimikaji mtambo wa kutibia maji, ujenzi wa vibanda vya kuendesha visima, ujenzi wa uzio katika tanki, kusogeza umeme na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji.

“DUWASA inaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuisaidia upatikanaji fedha za kutekeleza miradi ya majisafi, uondoshaji majitaka jijini Dodoma na kuendelea kutatua changamoto ya upatikanaji huduma hizo maeneo mbalimbali jijini Dodoma,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Antony Sanga, aliimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *