
Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe awasili mkoani Tabora asubuhi ya leo tarehe 2 Julai, 2022 na kupokelewa na Katibu Tawala wa mkoa wa Tabora Bwana Msalika oMakungu pamoja na Mkuu wa wilaya ya Tabora Mjini, Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda tayari, kuhitimisha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Dunia mwaka 2022 (SUD).
Akiwa katika uwanja wa ndege wa Tabora, Waziri Bashe ametoa agizo kwa Uongozi wa mkoa (RAS Tabora, Mkuu wa Wilaya) pamoja na Mrajis Msaidizi Tabora kuanzia msimu huu wa kilimo tumbaku ya Wakulima inunuliwe kwa wakati badala ya kusubiri kwa zaidi ya miezi mitatu tangu kuvunwa.
“Turuhusu ushindani ili tumbaku inunuliwe haraka, kwa mfano kuna mnunuzi (Kampuni ya Mkwawa Leaf Tobacco) yupo tayali kununua tumbaku kutoka kwa Wakulima, tujenge mazingira mazuri kwa Wanunuzi”. Amesisitiza Waziri Bashe.

Aidha; Waziri Bashe ameongeza kuwa kuanzia sasa, uwekwe utaratibu wa kuanzisha masoko kwenye maeneo ya Wakulima tofauti na ilivyo sasa ambapo masoko yapo mbali na maeneo ya Wakulima.
“Mkulima wa wilaya ya Kaliua awekewe utaratibu wa kufuatwa huko huko alipo na si kumpa mzigo wa kusubiri tumbaku yake isafirishwe kutoka eneo moja kwenda eneo lingine.
Wakati huo huo; Waziri Bashe pia ametoa agizo kwa Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku (TORITA) kuanzia msimu ujao wa kilimo, kugawa mbegu bora za tumbaku kwa Wakulima ili waongeze tija na uzalishaji.
