BONANZA LA KUWAAGA WASTAAFU TUME YA MADINI LAFANA

  • Michezo ni Afya tushirikiane kwa pamoja

Imeelezwa kuwa, michezo inaleta afya, akili , urafiki na kuwaweka pamoja Wafanyakazi wa Tume ya Madini.

Hayo yamebainishwa leo Julai 2, 2022 na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula wakati wa ufunguzi wa Bonanza ya kuwaaga Wastaafu wa Tume ya Madini lililofanyika katika Viwanja vya Kilimani, Jijini Dodoma.

“Nawapongeza Wafanyakazi wote kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika michezo mbalimbali , tuendelee kufanya mazoezi ili tuweze kupata nguvu ya kuendelea kufanya kazi ya kulinda rasilimali zetu na kukuza Uchumi wa Nchi,” amesema Prof. Kikula.

Prof. Kikula amesema kuwa tuendelee kushirikiana ili kufikia lengo la makusanya tulilopangiwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ya bilioni 822.

“Bila ushirikiano kwa wafanyakazi hatuwezi kufika kokote nashukuru uadilifu wenu unaonesha wazi kuwa tulipopangiwa kukusanya maduhuli tumefika asilimia 96 na zaidi,” amesema prof kikula.

Vilevile, Prof. Kikula amewapongeza washiriki wa Bonanza na kuwataka waendelee kufanya mazoezi mara kwa mara maana michezo ni furaha.

Naye, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema Mhe. Rais Mama Samia Suluhu Hassan, anawasisitiza watu kufanya mazoezi kwa kuwa ni moja kati ya kinga ya kuufanya mwili kuwa imara ili kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

Pia, alisisitiza Watumishi wa Tume ya Madini kuwa na umoja na kutojibweteka katika kazi ili kuendelea kuleta matokeo chanya kwenye Sekta ya Madini na kuzidi kufikia malengo ya kukusanya maduhuli yanayowekwa na Serikali.

“Ninyi msipokuwa waadilifu, msipopendana na kuwa na ushirikiano Tume ya Madini haipo, kikubwa katika ushiriki wa bonanza hili ni kutufanya tuwe kitu kimoja,” amesema Samamba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Tume, CPA. William Mtinya amesema kuwa mazoezi ni afya, rai yangu tusiache mazoezi tushirikiane na kuwa pamoja.

Aidha, Kaimu Meneja wa Ukaguzi fedha,Kodi na Ushirikishwaji wa Watanzania, Geoffrey Nsemwa amewasilisha kwa ufupi umuhimu wa Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye Sekta ya Madini kwenye bonanza ya kuwaaga Wastaafu ili kuwawezesha wafanyakazi wa Tume ya Madini kujua maana ya Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye Sekta hiyo.

Vilevile, katika Bonanza la kuwaaga Wastaafu Mwasilishaji kutoka PSSF, Juma Venerando ameeleza mambo machache kuhusu wajibu wa wadau, mafao na michango kwa Wastaafu na Wafanyakazi wa Tume ya Madini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *